Chama cha wanasheria nchini kimejiunga na washikadau wengine nchini na viongozi kuishinikiza huduma ya polisi kutoa maelezo kuhusu visa vya utekaji nyara ambavyo vimeripotiwa nchini katika wiki moja iliyopita.
Viongozi wa upinzani na baadhi ya viongozi serikalini wamekuwa wakishinikiza asasi za usalama za huduma ya kitaifa ya polisi na idara ya upepelezi ya makosa ya jinai DCI kutoa taarifa kamili kuhusu kuliko vijana ambao wanadaiwa kutoweka kwa kutekwa nyara hadharani na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, LSK imeelezea wasiwasi wake kufuatia ongezeko la kupotea kwa vijana ikitaja visa hivyo kuwa vya kutoweka kwa lazima kwa vijana na ukiukaji wa haki za kibinadamu zinazolenga haswa vijana wanaotumia mtandao.
LSK imetaka NPS kutoa maelezo ya waliko vijana Billy Mwangi, Peter Muteti, Benard Kavuli na ripoti za kuzuiliwa kwa Gabriel Supeet anayedaiwa kuwa anazuiwa katika kituo cha polisi cha Ntulele.
Chama hicho kinachoongozwa na Faith Odhiambo, kwa kujibu taarifa ya huduma ya polisi iliyokana kuhusika kwa maafisa wake katika utekaji nyara, LSK imeitaka NPS kuchunguza na kuwawajibisha watu wanaohusika na utekaji nyara, Kuhakikishia umma usalama wake kwa kuchukua hatua madhubuti na zinazoonekana kulinda wananchi dhidi ya utovu wa usalama na kufanya kazi na asasi nyingine za usalama ilikurejesha Imani ya wananchi.
LSK imewashauri wananchi ambao wapendwa wao wametoweka kwa njia tatanishi kuwa na habari za kuaminika kuhusu waliotekwa na kuwasilisha malalamishi kwa LSK kupitia matawi yake kote nchini.
Chama hicho kimemtaka inspekta jenerali wa polisi kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha usalama wa wananchi wote la sivyo ajiuzulu kwenye majukumu hayo.
LSK imeonya kwamba ikiwa NPS itakosa kuchukua hatua
madhubuti kunahatarisha kuwatia moyo wahalifu na kukuza utamaduni wa kutokujali,
jambo ambalo moja kwa moja linakiuka haki za binadamu, katiba na mwongozo wa
sheria.