Mkuu wa Uchumi wa Ubunifu na Miradi Maalum katika Afisi Kuu ya Rais, Denis Itumbi, amepuuzilia mbali tetesi za mtafaruku kati ya Rais William Ruto na naibu wake Kithure Kindiki.
Katika siku za hivi majuzi kumekuwa na uvumi kwamba viongozi hao wawili wanaoshikilia viti vya juu zaidi nchini huenda tayari wametofautiana. Uvumi huo ulionekana kuenezwa zaidi baada ya naibu wa rais kukosekana kwenye mkutano wa mkesha wa Mwaka Mpya uliofanyika katika Kisii State Lodge usiku wa kuamkia Januari 1, 2025.
Katika taarifa yakesiku ya Jumatano jioni, Itumbi alibainishakuwa kinyume na madai hayo, rais na naibu wake wanashirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa manifesto ya Kenya Kwanza.
“Rais na naibu wake wanashughulika kutekeleza MPANGO. Mwaka huu miradi na programu zitazungumza. Mnamo 2025, tutaonyesha UONGO kwa wakati halisi,” Itumbi alisema kupitia mitandao ya kijamii.
Mwanahabari huyo pia alitupilia mbali madai ya mabishano ya hivi majuzi kati ya DP Kindiki na msaidizi wa Rais Ruto Farouk Kibet.
“Ati DP @KindikiKithure alipigwa kofi na Farouk. UWONGO. Ati kuna mtafaruku, tafadhali andika UWONGO, hiyo inadumu,” alisema.
Jioni ya Desemba 31, 2024, naibu wa rais Kithure Kindiki hakuonekana mahali popote kwenye kikao cha chakula cha jioni cha mkesha wa Mwaka Mpya kilichofanyika Kisii State Lodge. Hili sio la kawaida na lilizua tetesi za mzozo kati ya watendaji wakuu huku Wakenya hata wakikisia ulikoanzia.
Haya yanajiri miezi miwili tu baada ya aliyekuwa waziri wa maswala ya ndani kuchukua wadhifa wa Rigathi Gachagua ambaye alitimuliwa kama naibu rais wa Kenya katikati ya mwezi wa Oktoba.