logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Maelezo mapya kuhusu kifo cha Ibrahim Mwiti yaibuka, familia yasema hakuwa mwanaharakati

Polisi wamepuuzilia mbali madai kwamba Ibrahim alitekwa nyara kabla ya kupatikana amefariki.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri05 January 2025 - 11:50

Muhtasari


  • Polisi walibainisha kuwa ripoti kuhusu kutekwa nyara kwa Ibrahim si za kweli na wakafichua matokeo ya uchunguzi wao.
  • Polisi wamesema mama wa kijana huyo alirekodi taarifa akisema kuwa mwanawe sio mwanaharakati.


Tume ya Huduma ya Kitaifa kwa Polisi (NPS) imepuuzilia mbali madai kwamba kijana Ibrahim Hilal Mwiti alitekwa nyara kabla ya kupatikana amefariki.

Katika taarifa ya Jumatatu asubuhi, polisi walibainisha kuwa ripoti kuhusu kutekwa nyara kwa Ibrahim si za kweli na wakafichua matokeo ya uchunguzi wao.

Walisema kutokana na uchunguzi wao, marehemu Ibrahim alionekana akiwa hai mara ya mwisho mnamo Novemba 11, 2024 kabla ya mama yake kutoa taarifa kuhusu mtu aliyepotea katika Kituo cha Polisi cha Juja mnamo Novemba 15, 2024.

Walidai kuwa mwili wa kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 ulipatikana mnamo Novemba 12, 2024 usiku wa manane na Polisi wa Trafiki wa Juja baada ya kudaiwa kugongwa na gari lililotoweka alipokuwa akiendesha pikipiki katika eneo la Spur Mall kwenye Thika Super Highway.

"Mwili huo uliokuwa na majeraha kichwani ulisafirishwa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya General Kago kama mtu asiyejulikana kutokana na ukosefu wa vitambulisho katika eneo la ajali, na pikipiki ilihifadhiwa katika Ofisi ya Trafiki ya Juja," taarifa hiyo ilisema.

“Alama za vidole vya marehemu zilichukuliwa na Polisi wa Trafiki wa Juja, zikawasilishwa Ofisi ya Taifa ya Usajili, na matokeo ya Novemba 21, 2024, yalibainisha kuwa mwili wa marehemu ni wa Ibrahim Hilal Mwiti. Januari 2, 2025, mama yake Ibrahim alichukua hati ya kiapo mbele ya Mahakama za Sheria za Thika kuomba kuachiliwa kwa uchunguzi wa postmortem kwa mujibu wa imani yake ya kidini, na baadaye walitaka kuachiliwa kwa mwili huo ambao ulikubaliwa na Mahakama Mwili huo ulizikwa katika Makaburi ya Waislam ya Lang'ata Januari 3, 2025."

Polisi pia walisema kuwa mama wa kijana huyo alirekodi taarifa mnamo Januari 4, 2025 ikisema kuwa mwanawe sio mwanaharakati kama ilivyodaiwa.

“Huduma ya Polisi ya Kitaifa inavitaka vyombo vya habari na umma kwa ujumla kujiepusha na kusambaza habari ambazo hazijathibitishwa na za kupotosha, zinazoweza kuwachochea wananchi,” walisema.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved