Katika uchaguzi huo chama chake John Mahama cha National Democratic Congress {NDC} ilipata ushindi wa asilimia 56.55% za kura huku chama cha New Partriotic Party wakipata asilimia 41.61%. uchaguzi huo ulikuwa wa kihistoria kwani ni mara ya kwanza nchi ya Ghana ilipata naibu rais wa kike tangia enzi ya uhuru.. Naana Jane Opoku –Agyemang atakumbukwa kama naibu rais wa kwanza kike wa Ghana.
Mahama alichaguliwa katika uchaguzi wa Desemba 2012 kuhudumu kama rais na kuhudumu mpaka mwaka wa 2016, ambapo aligombea kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili katika uchaguzi wa 2016, lakini akashindwa na mgombeaji wa New Patriotic Party Nana Akufo-Addo. Hii ilimfanya kuwa rais wa kwanza katika historia ya Ghana kutoshinda muhula wa pili mfululizo.
Baadaye Mahama alikuwa tena mgombea wa urais wa chama cha NDC katika uchaguzi wa mwaka wa 2020, ambapo alishindwa na Akufo-Addo kwa mara ya pili.
Aidha, hafla hiyo ya uapisho wake iliwaleta pamoja wageni wengi kutoka Ghana wakiwemo makamu wawili wa rais, spika mmoja wa bunge, marais wawili wa zamani, na wakuu kadhaa wa mashirika ya kimataifa, wakiwemo wawakilishi kutoka jumuiya ya madola na benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB).
Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu, Rais wa Kenya William Ruto ni miongoni mwa viongozi 21 wa nchi mbalimbali waliofika kushuhudia hafla hiyo ya kihistoria katika nchi ya Ghana pamoja na wajumbe kutoka umoja wa ulaya, Marekani na Uingereza.
Katika hotuba yake ya kuapishwa, Rais John Dramani Mahama alielezea maono yake ya ufufuaji wa uchumi wa Ghana, ushirikishwaji, na mageuzi ya utawala. Aliwahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kwamba Ghana iko wazi kwa biashara tena, akiahidi mfumo wa kodi ulio wazi na wa haki ili kuchochea ukuaji.
‘’Tutarekebisha mifumo yetu ya ushuru ili kuifanya iwe ya haki na uwazi. Jumuiya ya wafanyabiashara lazima ijue kwamba Ghana imerejea katika biashara, tunahitaji kuweka upya imani katika nchi yetu, katika taasisi zetu na sisi wenyewe. Wewe ni Ghana, mimi ni Ghana. Kwa pamoja tunaifanya nchi hii kuwa bora. Hebu tuingie katika agano la kujenga Ghana tunayotamani sote.” Alisema Dramani.
Alitoa wito kwa wananchi kuwa na maono ya Ghana wanayotaka kuiacha nyuma kwa ajili ya vizazi vijavyo, akihimiza mabadiliko ya mitazamo, tabia na fikra ili kufikia maendeleo ya pamoja.