Waziri wa elimu Julius Ogamba amesema serikali kufikia sasa
imejenga madarasa 14,500 kwa ajili ya kundi la kwanza la wanafunzi
wa gredi ya 9.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika Jumba la Mitihani huko South C akitangaza matokeo ya mtihani ya kitaifa ya kidato cha nne ya mwaka wa 2024. Ogamba alisema wanatazamia kufikia madarasa 16,000 kufikia mwisho mwa mwezi Januari.
‘’Hii imewezekana kutokana na serikali kutoa shilingi bilioni 11 kwa shule kote nchini kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 11,000 wanafunzi wa daraja la 9,’’ Alisema Ogamba.
Ogamba aliendelea kueleza kuwa shilingi bilioni 6.8 zaidi zilitengewa maendeleo ya maeneo bunge na bilioni 3.4 kutoka wizara ya elimu na bilioni 3.4 kutoka kwa fedha za maendeleo ya maeneo bunge na kwa ajili ya kujenga madarasa 6,800.
Waziri huyo aliwapongeza wabunge kwa ushirikiano wao mkubwa na juhudi zao katika ujenzi wa madarasa vya shule sekondari msingi. Aliongeza kuwa wizara itajenga madarasa zaidi 7,290 ili kukabiliana na ongezeko la usajili wa wanafunzi ili kuhakikisha mabadiliko mazuri kwa kundi hilo.
Ogamba alitangaza kuwa serikali imeshinda changamoto zinazotarajiwa katika juhudi za kuwaweka wanafunzi wote wa 2024 wa gredi ya 8 katika madarasa ya gredi ya 9, kiwango cha juu zaidi cha sekondari msingi.
Awali siku ya mnamo Jumanne, waziri alisema wizara, kupitia ushirikiano na mashirika mengine inafanya kila iwezalo kuhakikisha mabadiliko ya daraja la 9.
"Pale ambapo kuna changamoto, inafaa kutiliwa mkazo, na suluhu ipatikane, ikiwa ni pamoja na kuunganisha madarasa kwa madaraja ya chini ili wanafunzi wa darasa la tisa wasiathirike," Alisema Ogamba.
Kuhusiana na suala la vitabu Ogamba aliongeza kuwa wizara imenunua vitabu 9,926,618 vya gredi ya 9, ambavyo vimegawiwa shule huku ugavi wa huo ukitarajiwa kukamilika mwishoni mwa Januari.
‘’Nimeagiza taasisi ya ukuzaji mtaala ya Kenya kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuwa vitabu vyote vinavyohitajika na vifaa vingine vya kufundishia vinapatikana kwa matumizi ya wanafunzi wetu,” Aliongeza Ogamba.
Serikali kupitia wizari ya elimu inafanya bidii kwa kuwahakikishia walimu, wanafunzi na wazazi kuwa mtaala mpya wa masomo nchini uko imara na kujiandaa ipasavyo kusuluhisha changamoto zote zitakazozuka.