Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Anne Kananu na mbunge mteule
Wilson Sossion ni miongoni mwa wagombeaji 109 ambao wameorodheshwa na tume ya
utumishi wa umma kwa nafasi za katibu mkuu.
Wengine walioteuliwa ni aliyekuwa katibu mkuu wa muungano wa madaktari, wafamasia na madaktari wa meno (KMPDU) Oluga Fredrick Ouma, aliyekuwa katibu mkuu wa utawala David Michael Otieno Osiany na mchambuzi wa mitandao ya kijamii Gabriel Oguda.
Tume ya utumishi ya umma ilitangaza kufunguliwa kwa nafasi ya kuomba kazi ya makatibu wakuu mnamo Novemba 20, 2024, kuashiria uwezekano wa mabadiliko kufanyika katika sekta hiyo.
Watu waliopendezwa na nafasi hizo walikuwa na hadi Desemba 4, 2024, kuwasilisha maombi yao.
“Kifungu cha 155(3)(a) cha katiba ya Kenya, 2010, kinaamuru tume ya utumishi wa umma kupendekeza watu binafsi kwa ajili ya kuteuliwa kuwa makatibu wakuu. Kulingana na kifungu hiki cha kikatiba, tume ya utumishi ya umma inakaribisha maombi kutoka kwa wagombeaji waliohitimu kwa nafasi ya katibu mkuu,” Hii ni kutokana na mujibu wa tangazo hilo lililochapishwa na tume ya utumishi ya umma.
Jumla ya wakenya 2,517 waliomba nafasi hizo, kulingana na tume hiyo lakini ni majina ya watu 109 pekee ndio waliorodheshwa na tume hiyo.
Wagombea walioteuliwa watahojiwa katika afisi ya tume ya utumishi wa umma, nje ya Harambee Avenue Nairobi kwa tarehe na saa ambayo itachapishwa kwenye tovuti ya tume hiyo baadaye.
Tume hiyo imewaalika umma kutoa taarifa zozote za kuaminika za maslahi zinazohusiana na wagombeaji walioorodheshwa (kupitia hati za kiapo) kwa Katibu/ mkurugenzi mtendaji, tume ya utumishi wa umma au mtandaoni kupitia [email protected] ili ipokewe kabla au Januari 24, 2025.
Mwenyekiti wa tume hiyo Antonny Muchiri alisema kuwa nafasi hizo zilitokana na kupangiwa kazi nyingine ndani ya nyadhifa mbalimbali za watendaji, na hivyo kusababisha hitaji la makatibu wakuu wapya.
Tume iliainisha mahitaji ya kuomba kazi hiyo kuwa ni pamoja na uelewa wa jumla wa shughuli za serikali, uwezo unaoonekana wa uongozi na usimamizi, na kufuata sura ya Sita ya katiba kuhusu uongozi na uadilifu.
Wagombea watakaofaulu watachukua jukumu la afisa mhasibu wa Idara ya Jimbo, kusimamia rasilimali za kifedha na watu, na kuhakikisha maendeleo na utekelezaji wa mifumo ya utendaji.