Familia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta inaomboleza kifo cha binamu yake Kibathi Muigai.
Kibathi, ambaye alikuwa dereva wa magari ya kushindana mbio, inasemekana alifariki wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 72.
"Kwa huzuni na kukubali mapenzi ya Mungu, tunatangaza kufariki kwa Kibathi Muigai mnamo Januari 10, 2025," tangazo katika mojawapo ya magazeti ya kila siku ya humu nchini lilisomeka.
Hata hivyo, hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu sababu ya kifo chake.
Kibathi, anayejulikana kama Wa Ngina pia alikuwa mfanyabiashara maarufu kutoka kwa familia kubwa ya Kenyatta.
Marehemu alikuwa ndugu wa wanasiasa Beth Mugo, Ngengi Muigai na Kungu Muigai.
Kungu ndiye msimamizi wa Kiama Kiama, kikundi kinacholeta pamoja wazee kutoka jamii za Mlima Kenya.
Kwa sasa anahudumu kama mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kituo cha Utamaduni cha Kenya baada ya kuteuliwa Januari 2023.
Anajulikana kuwa mfuasi mkubwa wa Rais William Ruto.
Wakati wake kama dereva wa safari za hadhara, Kibathi aliendesha gari aina ya Mitsubishi Colt Lancer huku baharia wake akiwa Arshad Khan.
Dereva nyota huyo wa Mitsubishi alikuwa sawa na Joginder Singh almaarufu ‘Flying Sikh” ambaye alishinda mashindano hayo mara tatu.
Anatazamiwa kuzikwa Ijumaa nyumbani kwake Ichaweri, eneo la Gatundu Kusini.
Kulingana na familia, mhudumu huyo ataondoka katika mochari ya Lee asubuhi na ibada ya mazishi ikipangwa kuendeshwa siku hiyo hiyo katika kanisa la Nairobi Chapel, Barabara ya Ngong.
Marehemu ameacha mke Josephine Nduta na watoto saba.