Naibu rais Kithure Kindiki amewaonya viongozi kutoka Embu
dhidi ya siasa ya uchochezi na vurugu akizungumza Ijumaa 17 januari, 2025 alipowakaribisha
wakaazi 1500 kutoka kaunti ya Embu katika makazi yake rasmi Karen.
Kindiki alisema kuwa vurugu na uchochezi ni njia hatari ya kisiasa na ni tofauti na tabia ya kawaida ya watu wa Kaunti ya Embu anaowajua.
Naibu rais alisisitiza kuwa amekuwa akitumia njia ya Embu tangu alipokuwa katika Shule ya upili na hajawahi kuona tabia kama hiyo miongoni mwa wakazi hao.
“Nimepitia mji wa Embu tangu nikiwa mvulana na sijawahi kuona barabara hiyo imefungwa kwa mawe na watoto wa Embu wakirusha mawe kuharibu maduka ya watu waliojenga vitega uchumi vyao na kuajiri vijana wetu wachache, naomba tuwache tabia hiyo,’’ Alisema Kindiki.
Matamshi yake yanajiri wiki chache baada ya maandamano kushuhudiwa katika mji wa Embu, ambako wakazi walitaka Billy Mwangi aliyedaiwa kutekwa nyara aachiliwe.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alichukuliwa kwa nguvu na watu wasiobainika kutoka kwa kinyozi huko Embu mnamo Jumamosi 21 Desemba 2024.
Wakazi walichoma tairi, kufunga barabara na kuharibu mali wakati wa maandamano hayo.
Kando na hayo Kindiki vilevile aliwahakikishia wakenya kuwa hakuna sehemu ya nchi yoyote itakayobaguliwa wakati serikali ikiharakisha kukamilisha miradi muhimu nchini.
‘’Tunaibeba nchi nzima, tunataka kuhakikisha kuwa hakuna sehemu ya nchi inayoachwa nyuma. Uongozi sio kupendelea mmoja kuliko mwingine. Inabeba kila mtu," Alisema Kindiki.
Naibu rais alisema mchango wa wananchi katika kile kinachofanywa katika kaunti ni muhimu, hivyo kuwahimiza wakazi wa Embu kutambua vipaumbele na mipango ya maendeleo na kuyaangalia kwa makini ili kuhakikisha utimilifu wa haraka.
‘’Ni vyema kukutana na kufanya mazungumzo na wananchi. Mkutano huu ni wa kujadili vipaumbele vya maendeleo pekee na jinsi ya kusonga mbele kaunti zetu. Nitakutana na wajumbe mbalimbali kutoka kaunti zote na kufanya majadiliano sawa na haya," Aliongeza kindiki.
Akiwahutubia Kindiki alisisitiza kuwa ni lazima wananchi wasiingizwe kwenye vita vya kisiasa akisema kuwa wale wanaozingatia siasa kwa wakati huu wanapasawa kusubiri mpaka wakati mwafaka wa siasa.
Alisema kuwa kaunti ya Embu imekuwa ikifaidika kutokana na
miradi ya maendeleo ikiwemo mradi ya barabara, ukulima na ata nguvu za umeme.
Baadaye aliwaomba wakazi wa Embu kumkazia na kumuuliza kile ambacho atakuwa amewafanyia baadaye.