Sarah Wairimu anatarajiwa kortini leo Ijumaa
kujibu mashtaka mapya ya mauaji ya marehemu mumewe Tob Cohen.
Wairimu alikamatwa tena siku ya Alhamisi baada ya DPP Renson Igonga kusema sasa wana ushahidi mwingi unaoonyesha kuwa Wairimu alimuua Cohen usiku wa Julai 19 na 20, 2019, katika eneo la Lower Kabete, Kaunti ya Nairobi.
"Kufikishwa mahakamani kwa Wairimu kufuatia kukamatwa kwake Januari 23, kunakuja baada ya kupokea taarifa mpya kuhusiana na kifo cha Cohen kutoka kwa DCI," alisema DPP katika taarifa iliyosambazwa kwenye akaunti yao ya X.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa pamoja na
taarifa hizo mpya, DPP alitoa maombi ya kusitishwa kwa uchunguzi wa mauaji hayo
ambayo yalikubaliwa.
"Baada ya kukagua kwa kina nyenzo mpya, DPP ameridhika kwamba Wairimu alihusika katika kifo cha Tob Cohen," inaongeza taarifa yao.
DPP wa zamani Noordin Haji mnamo 2022
alifuta shtaka la mauaji na kupendekeza kesi hiyo isajiliwe kama uchunguzi.
Haji alihusisha uamuzi huo na wachunguzi kadhaa kutokwenda sawa.
Alisema kufungua uchunguzi wa umma kutaruhusu umma kutoa taarifa zozote muhimu kuhusu mauaji ya Cohen kwa mamlaka, kama inavyotakiwa na Sheria.
"DPP aliamua uchunguzi ufanyike kwa umma kwa lengo la kubaini watu waliohusika na mauaji ya marehemu Tob Cohen. Uchunguzi huo wa hadhara unatoa jukwaa kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kutengua mauaji hayo ili kupata taarifa hizo. kupitia mchakato wa mahakama," ODPP ilisema.