Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha
ya Marekani (ICE) imekanusha madai ya kuwalipa watu ili kuwaripoti wahamiaji
haramu.
Kumekuwa na uvumi unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuwa watu wanazawadiwa dola 750 (Sh97,000) wanapounga mkono malengo yanayoendelea ya utekelezaji wa uhamiaji wa raia kwa kuripoti wahamiaji ambao wako nchini humo kinyume cha sheria.
Katika taarifa yake siku ya Ijumaa hata hivyo, idara ya uhamiaji ya Marekani hata hivyo ilikanusha kutoa zawadi yoyote kwa taarifa kuhusu wahamiaji haramu.
"Kwa rekodi, kinyume na uvumi, ICE haitoi zawadi ya $750 kwa vidokezo vya kuunga mkono malengo ya utekelezaji wa uhamiaji," Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha ya Marekani ilisema.
Uvumi kuhusu zawadi hizo za fedha uliibuka siku chache zilizopita baada ya rais Donald Trump kutangaza vita dhidi ya wahamiaji haramu nchini Marekani.
Kulikuwa na madai katika mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya Wakenya wanaoishi nchini Marekani walihusika kikamilifu katika kuwaripoti Wakenya wenzao ambao wako katika nchi hiyo ya Magharibi bila stakabadhi zinazohitajika.
Mamia ya wahamiaji haramu nchini Marekani walikamatwa Alhamisi na mamia ya wengine walisafirishwa nje ya nchi hiyo kwa ndege za kijeshi huku oparesheni ya Rais Trump ya kuwahamisha raia wengi ikiendelea, Ikulu ya Marekani ilisema.
Katika chapisho la X mnamo Alhamisi usiku, katibu wa habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt alisema, "Utawala wa Trump ulikamata wahalifu haramu 538 akiwemo mshukiwa wa kigaidi, wanachama wanne wa genge la Tren de Aragua, na wahalifu kadhaa waliopatikana na hatia ya uhalifu wa ngono dhidi ya watoto. "
Waliokamatwa 538 ni pamoja na watu 373 wenye rekodi za uhalifu na watu 165 wasio na rekodi za uhalifu kando na ukiukaji wa uhamiaji, kulingana na nyaraka zilizotolewa na afisa mkuu wa utawala.
Watu wengine 1,041 waliondolewa au kurejeshwa makwao, kulingana na rekodi hizo.