Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) limevunja kimya kuhusu mustakabali wa wafanyakazi wake baada ya hatua mpya iliyochukuliwa na Rais Donald Trump ya kusitisha ufadhili wa wakala huo wa serikali ambao kimsingi una jukumu la kusimamia misaada ya kiraia kutoka nje na usaidizi wa maendeleo.
Kupitia taarifa rasmi, USAID imetangaza kuwa kuanzia Ijumaa, Februari 7, 2025, mwendo wa saa tano na dakika 59 usiku (saa za Marekani), wafanyakazi wake wa moja kwa moja kote duniani watawekwa kwenye likizo ya kiutawala, isipokuwa wale waliochaguliwa kushughulikia majukumu muhimu.
"Kuanzia Ijumaa, Februari 7, 2025, saa 5:59 usiku (EST), wafanyakazi wote wa USAID walioajiriwa moja kwa moja watawekwa kwenye likizo ya kiutawala kimataifa, isipokuwa wale walioteuliwa kwa kazi muhimu," inasema taarifa ya USAID.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wafanyakazi waliotarajiwa kuendelea na kazi watajulishwa kufikia siku ya Alhamisi, Februari 6, 2025.
Kwa wafanyakazi wa USAID walioko nje ya Marekani, shirika hilo limetangaza kuwa, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, linaandaa mpango wa kuwarejesha nyumbani ndani ya siku 30.
Pia, mikataba ya wafanyakazi wa kimkataba (PSC na ISC) ambao hawatahitajika tena itasitishwa siku ya Ijumaa..
USAID pia imetangaza kuwa itazingatia kesi za kipekee kwa wafanyakazi wanaohitaji muda zaidi kabla ya kurejea Marekani.
“Shirika litaangalia kila kesi kwa umakini, hasa kwa wafanyakazi wenye changamoto za kiafya, ujauzito, au masuala ya kifamilia kama vile kuhitimisha muhula wa masomo wa watoto wao,” taarifa hiyo imeeleza.
Hatua hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa Kenya, ambako USAID inafadhili miradi mingi ya maendeleo, hasa katika sekta za afya, elimu, na kilimo.
Ikiwa baadhi ya wafanyakazi wa USAID wataondolewa au mikataba yao kusitishwa, miradi hiyo inaweza kuathirika, jambo litakaloathiri jamii zinazotegemea ufadhili huo.
Serikali ya Kenya na washirika wa maendeleo huenda wakalazimika kutafuta njia mbadala ili kuhakikisha kuwa miradi ya USAID inaendelea bila kuathirika kwa kiasi kikubwa.
Katika kumalizia, USAID imewashukuru wafanyakazi wake kwa huduma yao na kuahidi kutoa mwongozo zaidi katika siku zijazo.