Rais wa Marekani Donald Trump jana Alhamisi (Feb 7) aliidhinisha vikwazo vya kiuchumi na usafiri vinavyowalenga watu wanaofanya uchunguzi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya raia wa Marekani au washirika wa Marekani kama vile Israel.
Hii siyo mara ya kwanza ya rais Donald Trump, kuchukua hatua kama hizi kwani amerejelea uamuzi wake wa awali ambao alikuwa amechua katika muhula wake wa kwanza.
ICC siku ya Ijumaa ililaani vikwazo hivyo na kutoa wito kwa nchi wanachama 125 kuunga mkono wafanyakazi wake.
"Mahakama inasimama imara na wafanyakazi wake na kuahidi kuendelea kutoa haki na matumaini kwa mamilioni ya waathirika wasio na hatia wa ukatili duniani kote, katika hali zote kabla yake," ilisema taarifa hiyo.
Hatua hiyo ya Trump ilikwenda sambamba na ziara ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Waziri mkuu huyo pamoja na waziri wake wa zamani wa ulinzi na kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas - wanatafutwa na ICC kuhusiana na vita katika Ukanda wa Gaza nchini Israel.
Haijulikani ni kwa haraka kiasi gani ila Marekani huenda ikatangaza majina ya watu waliowekewa vikwazo.
Wakati wa utawala wa kwanza wa rais Trump mwaka 2020, Washington ilimwekea vikwazo mwendesha mashtaka wa wakati huo Fatou Bensouda na mmoja wa wasaidizi wake wa juu kuhusiana na uchunguzi wa ICC kuhusu madai ya uhalifu wa kivita unaofanywa na wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.
Vikwazo hivyo ni pamoja na kufungia mali yoyote ya Marekani kwa wale walioteuliwa na kuwazuia wao na familia zao kutembelea Marekani.
Uholanzi, taifa mwenyeji wa mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, imesema inajutia vikwazo hivyo.
"Kazi ya mahakama ni muhimu katika mapambano dhidi ya kutokujali," Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Caspar Veldkamp alisema katika chapisho la X.
Lakini Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, mshirika mkubwa wa Trump, alisema vikwazo hivyo vinaonyesha kuwa huenda ni wakati wa kuondoka ICC.
ICC ni mahakama ya kudumu ambayo inaweza kuwashtaki watu binafsi kwa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, mauaji ya kiholela, uhalifu na uchokozi dhidi ya eneo la nchi ya wanachama au na raia wao.
Marekani, China, Urusi na Israel sio wanachama.