logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mtangazaji Leonard Mambo Mbotela Amezikwa Katika Makaburi ya Lang'ata

Mbotela alifariki mnamo Februari 7, 2025.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri15 February 2025 - 15:23

Muhtasari


  • Mkewe, Alice Mambo, pamoja na mwanawe Jimmy na bintiye Ida, walikuwa miongoni mwa wanafamilia waliohudhuria mazishi.
  • Wanasiasa, wanahabari, wasanii, na watu wengine mashuhuri walijitokeza kusimama na familia yake.

Marehemu Leonard Mambo Mbotela alizikwa Jumamosi

Gwiji wa utangazaji Leonard Mambo Mbotela ambaye aliaga dunia wiki jana hatimaye amezikwa katika makaburi ya Lang’ata, kaunti ya Nairobi.

Mkewe, Alice Mambo, pamoja na mwanawe Jimmy na bintiye Ida, walikuwa miongoni mwa wanafamilia waliohudhuria mazishi hayo ya Jumamosi mchana.

Mamia ya waombolezaji walikusanyika katika makaburi ya Lang’ata, nyuso zao zikiwa zimejawa na huzuni, ili kutoa heshima zao za mwisho kwa mtangazaji ambaye sauti yake ilitawala mawimbi ya Kenya kwa miaka mingi.

Wanasiasa, wanahabari, wasanii, na watu wengine mashuhuri walijitokeza kusimama na familia yake, wakimheshimu gwiji ambaye mchango wake ulisaidia kuunda uandishi wa habari wa Kenya.

Miongoni mwa waliohudhuria ni mwakilishi wa wanawake wa Nairobi Esther Pasaris, mtangazaji mkongwe wa radio Fred Obachi Machoka, mwanamuziki John Katana wa The Mushrooms, na wanahabari mashuhuri Pauline Sheghu, Kipkoech Tanui, na Zubedah Kananu.

 Pia waliokuwepo kuenzi marehemu ni nguli wa soka Bobby Ogola na mwanahabari wa michezo Mike Otieno.

Mbotela alifariki mnamo Februari 7, 2025.

Mwanahabari huyo mkongwe alikuwa hajisikii vizuri kwa muda na alikata roho mwendo wa saa tatu unusu siku ya Ijumaa wiki iliyopita.

Ibada ya ukumbusho ya mtangazaji huyo mashuhuri ilifanyika Ijumaa katika Kanisa Kuu la All Saints Cathedral kuanzia saa nane mchana.

Familia, marafiki wa karibu, wafanyakazi wenzake wa zamani, wanasiasa na watu wengine mashuhuri walihudhuria ibada ya kumbukumbu iliyofanyika kumuenzi marehemu.

Mnamo Alhamisi, spika Moses Wetang’ula alisema inavunja moyo kwa mtangazaji Leonard Mambo Mbotela kuzikwa katika makaburi ya Lang’ata.

Akizungumza wakati wa kikao cha Bunge, spika alipendekeza haja ya nchi kuwa na makaburi maalumu ya kuzika mashujaa wa kitaifa.

Weta aliliomba Bunge kusimama na kuzingatia dakika za ukimya katika kumbukumbu ya mtangazaji aliyefariki.

“Nchi inahitaji sehemu maalum ya shujaa kuzika watu kama mtangazaji Leonard Mambo Mbotela, inakatisha tamaa kusikia kwamba tunaenda kumzika mtangazaji Leonard Mambo Mbotela katika makaburi ya Lang’ata; pengine kaburi lake litakuwa juu ya kaburi likijua jinsi eneo hilo lina watu wengi,” Wetang’ula alisema.

Mwanahabari huyo nguli alisifika kwa kipindi chake maarufu cha redio na TV Je Huuu ni Ungwana?, kilichopeperushwa kwenye redio na TV za KBC.

 Kipindi hichi kilifurahia kupeperushwa kwa takriban miaka 55.

Mbotela alifanya kazi kwa muda mfupi na Kenya Weekly News na East African Standard kabla ya kujiunga na KBC.


 


 Mwanahabari huyo mkongwe alizaliwa Freetown, Mombasa, mwaka wa 1940 na James na Aida Mbotela. Alikuwa mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto wanane.


 



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved