Spika wa kaunti ya Trukana Christopher Doye Nakuleu alijiuzulu Jumanne siku mbili kabla ya kujadiliwa mswada wa kumuondoa mamlakani kujadiliwa.
Mwakilishi wadi wa Kalolok Michael Ebenyo aliwasilisha bungeni mswada wa kumbandua ofisini spika huyo kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.
Kulingana na Nakuleu, alieleza kwamba amefanya mashauriano mapana na wapiga kura na wafuasi wake katika Kaunti nzima, ndipo akafikia hauta ya kujiuzulu.
"Ninaandika kujiuzulu rasmi kutoka nafasi yangu kama spika wa Bunge la Kaunti ya Turkana kuanzia Februari 25, 2025. Nimepata uzoefu wa thamani na kuunda uhusiano wa maana wakati wa mamlaka yangu. Uamuzi huu unakuja baada ya kuzingatia kwa makini malengo yangu binafsi na ya kitaaluma,"sehemu ya barua yake ilisoma.
Kujiuzulu kwake kunatajwa kama hatua ya busara kwani anapanga kujiandaa ili kupigania nafasi ya ugavana katika kauniti hiyo ili kumuondoa gavana wa sasa Jeremiah Ekamais Lomorukai mamlakani.
Wiki jana, angalau wawakilishi wadi wapatao 36 kati ya 46 waliunga mkono ombi lililowasilishwa kama hoja maalum ya kumuondoa spika madarakani sababu kuu zikitajwa kama ukiukaji wa katiba, utovu wa nidhamu na kutowajibika.
Kumekuwepo na madai kwamba uhusiano kati ya Nakuleu na Gavana wa kaunti hiyo ulianza kuzorota baada spika huyo kutaka kujua jinsi Fedha zilizokuwa zimetengwa ili kusaidia kununua chakula cha msaada kwa wenyeji zilivyotumika.
Nakuleu alimtaka Gavana aeleze kwa undani, mbona baadhi ya bidhaa hazikuwasilishwa kulingana na bajeti iliokuweko.
"Jukumu langu ni kusimamia na kuangalia utendaji. Bunge la Kaunti lilitenga milioni 551 kwa ajili ya ununuzi wa shehena kamili ya chakula cha msaada ikiwa ni pamoja na mahindi, maharagwe na mafuta ya kupikia mboga lakini hakuna maharagwe yaliyoletwa." alisema spika huyo, awali.
"Nyote mnafahamu kuna fumbo Turkana na jamhuri ya Kenya kuhusu sakata ya chakula cha msaada ambapo gavana hadi sasa hajatoa majibu kuhusu maharage hayo. Bosi wa Kaunti lazima awaambie watu wa Turkana mahali ambapo pesa za misaada zilikwenda." aliendea.
Kwa upande wake Gavana Lomorukai ametaja tetesi hizo kama propaganda za kisiasa tu. Alieleza kwamba walinunua magunia 119,000 ya mahindi na mafuta ila fedha hazikutosha kununua maharagwe.
"Kile ambacho spika anataka ni siasa za bei rahisi. Hatukuweza kujumuisha maharage katika bajeti ya chakula cha msaada kwa sababu MCAs walipunguza bajeti iliyopendekezwa kutoka milioni 700 hadi milioni 551,' alisema Gavana.