logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Rais William Ruto alizindua rasmi mashindano ya Safari Rally yanayofanyika mjini Naivasha

Rais William Ruto ameanzisha rasmi makala ya mwaka huu ya mashindano ya magari ya safari rally.

image
na Japheth Nyongesa

Yanayojiri21 March 2025 - 09:40

Muhtasari


  • Makala haya ya 72 ya Safari Rally yatajumuisha umbali wa kilomita 1,403.63.
  • Mradi huu pia unajumuisha utoaji wa michoro ya bure ya muundo wa magari ili kuhamasisha utengenezaji wa magari hapa nchini.

President William Ruto leading the opening of Safari rally at Naivasha

Rais William Ruto ameanzisha rasmi makala ya mwaka huu ya mashindano ya magari ya safari rally katika hafla iliyofanyika katika jumba la KICC hapa jijini Nairobi.

Jumla ya magari 37 yaliyojisajili yalielekea Kasarani kwa kituo cha kwanza cha mashindano saa saba hadi saa nane, kabla ya kuelekea Naivasha.

Makala haya ya 72 ya Safari Rally yatajumuisha umbali wa kilomita 1,403.63 zikiwemo 384.86 kupitia maeneo tofauti katika kaunti za Nakuru, Nairobi, na Kiambu za kuwania alama.

Toleo la mwaka huu linakuwa ndefu zaidi tangu kurejea kwa mashindano ya magari ya safari Rally kwenye kalenda ya WRC mwaka 2021.

Rally hii inajumuisha hatua mpya kama vile njia iliyo na sehemu ya mteremko ya kilomita 12.36 iliyojaa mashamba ya mizabibu, na Camp Moran, kipimo cha uvumilivu cha kilomita 32.2 kilichoundwa kwa lengo la kujaribu uwezo wa madereva bora wa rally duniani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio, Rais Ruto alisisitiza dhamira ya utawala wake ya kuunga mkono michezo ya magari, huku akionyesha azma ya kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali kuhusu tukio hili.

Alibainisha kuwa gharama za kuandaa rally zilipungua kutoka shilingi bilioni 2.1 mwaka 2023 hadi shilingi milioni 980 mwaka huu, kutokana na ufanisi zaidi katika uendeshaji na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.

“Natarajia wakati ambapo tukio hili litakuwa likigharimu serikali sifuri, huku sekta binafsi ikichukua umiliki kamili. Wanahitaji matangazo, uhamasishaji, na sisi tuko tayari kutoa nafasi kwa hilo,” alisema Rais Ruto.

Ili kukuza vipaji vya vijana katika michezo ya magari, serikali ya Kenya imeahidi kuunga mkono mradi wa FIA wa magari kwa bei nafuu, ambao unalenga kukuza vipaji vya madereva wachanga.

Mradi huu pia unajumuisha utoaji wa michoro ya bure ya muundo wa magari ili kuhamasisha utengenezaji wa magari hapa nchini.

Vilevile, Rais Ruto alikaribisha utekelezaji wa Mpango wa Kuvaa Kofia wa FIA, unaoendeshwa nchini Kenya na Chama cha Wamiliki wa Magari Nchini Kenya (AAK), ambao unatoa kofia za kuokoa maisha kwa waendesha boda-boda kama sehemu ya Mpango wa Usalama Barabarani wa Kitaifa wa 2024-2028.

Orodha ya washiriki ilitangazwa Ijumaa wiki iliyopita na inajumuisha madereva kutoka Kenya, Uingereza, Finland, Ubelgiji, Estonia, Japan, Ufaransa, Ireland, Ugiriki, Uswidi, Paraguay, Poland, Uhispania, Argentina, India, Tanzania na Uganda.

Mabingwa wa dunia Sebastien Ogier kutoka Ufaransa (mwaka 2013, 2014, 2015, 2016, 2017, 2018, 2020 na 2021), Kalle Rovanpera wa Finland (2022 na 2023), Ott Tanak kutoka Estonia (2019) na Mbelgiji Thierry Neuville (2024) pia wako katika orodha hiyo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved