Charles Nyachae, mwaniaji wa nafasi ya uwenyekiti wa IEBC, mnamo siku
ya Jumatatu Machi 24,2025 alisimulia jinsi alivyoonywa na watu mbalimbali
wakiwemo jamaa na marafiki dhidi ya kutuma barua ya maombi ya nafasi ya
uwenyekiti wa IEBC.
Alipojiwasilisha mbele ya jopo la uteuzi, Nyachae aliambia
jopo kuwa watu wengi walimpigia simu kumuuliza ikiwa alikuwa tayari kufa iwapo
angechaguliwa kama mwenyekiti wa IEBC na kumrithi mwendazake Wafula Chebukati.
Kulingana na usemi wa bwana Nyachae alisema kuwa hata
watu wake wa karibu walikuwa wakimuonya dhidi ya kukubali kutuma maombi kwa
nafasi hiyo, kulingana naye aliweza kujibu kwa kusema kuwa hakuwa tayari kufa wala
kupoteza maadili akihudumu katika nafasi hiyo.
Hatimaye Nyachae aliendelea kujipigia upato kwa
kujiiaminisha mbele ya jopo kuwa alikuwa muwaniaji bora zaidi kwa kuelezea yale
ambayo alitekeleza kabla.
‘’Mimi na wenzangu wengine wanane tulifanya kazi kama
wanachama wa jopo lililounda katiba ya Kenya ya mwaka wa 2010, azma ambayo
iliweza kufanikisha kila jambo kwa uzuri zaidi.
Nilipata fursa ya kufanya kazi na mtaalamu Daktari Koki
Muli kuhusu masuala ya uchaguzi ambapo niliweza kufaidi pakubwa kwa kujizolea
tajiriba pana’’Nyachae alieleza.
Aliendelea kwa kusema kuwa iwapo atachaguliwa na jopo kama
mwenyekiti wa tume atahakikisha kuwa
anafanya kazi kwa ushirikiano na makamishina wengine kwa ushirikiano wa
karibu na kuhakikisha kuwa anasikiliza maoni
na mahitaji ya kila mshikadau katika tume nzima.
Vilevile Nyachae aliweza kuelezea juhudi za kuhakikisha kuwa
suala la thuthi mbili katika uongozi linapewa kipaumbele kwa kuzingatia kuwa ni moja ya hitaji kuu la
Katiba na vyema zaidi ikiwa litafanikishwa.
Nyachae aliweza
kujieleza kwa kusema kuwa kasumba ambayo imekuwepo ya muda mrefu kutoka kwa wakenya ya kutoamini Tume ya IEBC ni wakati sasa lazima
mifumo ya kisheria iimarihwe na kuwe na uwazi kwa kila kitu kwanzia kwa uteuzi
wa mwenyekiti hadi siku ya kutangaza kwa matokeo ya uchaguzi.
Nyachae aliweza kusema kuwa ni fikra kuu ambazo zimekuwa zimejikita na kukolea miongoni mwa wakenya kwa kukosa Imani
na tume ya uchaguzi ila akasema yeye ni sehemu ya suluhisho iwapo atachaguliwa
na jopo kwa kuangazia uchapakzi wake wa hapo mbeleni.