
Polisi wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na mauaji ya kikatili ya Gaala Aden Abdi, msichana wa miaka 17 aliyepatikana ameuawa na mwili wake kuchomwa kwa sababu ya kukataa ndoa ya lazima na mwanamume mwenye umri wa miaka 55.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), Muchiri Nyaga, mwanamume huyo wa miaka 55, aliyepaswa kumwoa msichana huyo, ni miongoni mwa waliokamatwa.
“Tungependa kuthibitisha kuwa kufuatia kifo cha kusikitisha cha msichana huyu wa miaka 17, polisi waliweza kuchukua hatua za haraka na kuwatia mbaroni washukiwa watatu, akiwemo yule aliyekuwa akidai kuwa mume wa mtoto huyu,” alisema Nyaga katika taarifa yake Jumamosi.
Maafisa wa upelelezi wanaendelea kuchunguza mazingira ya mauaji haya huku mamlaka zikisisitiza haja ya kufanikisha uchunguzi bila upendeleo.
“Tunapaswa kuwaachia wachunguzi wafanye kazi yao kwa kina ili kubaini mazingira yote yaliyopelekea msiba huu wa kusikitisha. Huduma ya Polisi inaeleza masikitiko yake makubwa na tunatoa pole kwa familia ya marehemu,” aliongeza Nyaga.
Katika ujumbe wake kwa Wakenya, Nyaga alisisitiza haja ya kukataa tamaduni zinazowaweka watoto katika hatari, hasa ndoa za kulazimishwa.
“Tunaomba jamii kwa ujumla kuachana na desturi hatari na kuwaruhusu watoto waishi utoto wao ipasavyo,” alisema.
Washukiwa hao watatu wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu uchunguzi utakapokamilika.
Nyaga pia aliwashukuru wananchi waliotoa taarifa muhimu zilizosaidia katika kuwatia mbaroni washukiwa.
“Tunashukuru sana watu wote wa nia njema waliotoa fununu muhimu zilizochangia kukamatwa kwa washukiwa hawa,” alihitimisha.
Polisi wamerejelea dhamira yao ya kuhakikisha sheria inafuatwa huku uchunguzi ukiendelea.