4 wakamatwa kuhusiana na Sh94.9m za Quickmart zilizoibiwa na wafanyikazi wa Wells Fargo, Sh9.1m zapatikana

Ksh 9,101,300 zilipatikana kutokana na operesheni hiyo.

Muhtasari

•Wanne hao walikamatwa katika maeneo tofauti baada ya kuhusishwa na wizi huo ambao ulishtua taifa zima Jumatatu wiki jana.

•Washukiwa wawili walikamatwa walipokuwa wakilifanyia ukarabati gari linaloripotiwa kubeba pesa hizo, ili kuficha utambulisho wake.

wamekamatwa kuhusiana na Sh94.9 milioni za Quickmart zilizoibiwa.
Washukiwa 4 wamekamatwa kuhusiana na Sh94.9 milioni za Quickmart zilizoibiwa.
Image: TWITTER// NPS

Wapelelezi kutoka Kurugenzi ya Makosa ya Jinai (DCI)  ambao wanashughulikia kesi ya Ksh 94,918,750 zinazodaiwa kuibwa na wafanyikazi wa kampuni ya ulinzi wa fedha ya Wells Fargo siku chache zilizopita wamefanikiwa kuwakamata washukiwa wanne.

Wanne hao walikamatwa katika maeneo tofauti baada ya kuhusishwa na wizi huo ambao ulishtua taifa zima Jumatatu wiki jana. Ksh 9,101,300 zilipatikana kutokana na operesheni hiyo.

Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), mshukiwa wa kwanza, Ismael Patrick Gitonga alikamatwa katika eneo la Rongai, Kaunti ya Kajiado baada ya kubainika kuwa gari lake aina ya Toyota Fielder lilitumiwa kubeba pesa zilizoibwa kutoka kwa gari la kusindikiza lililokuwa limezibeba.

Gitonga pia anaripotiwa kuwa ndiye aliyeendesha gari hilo baada ya kuchukua pesa hizo.

Washukiwa wengine wawili, Michael Matolo Njeru na Samwel Onyango walikamatwa katika eneo la Njiru, jijini Nairobi walipokuwa katika harakati za kulifanyia ukarabati gari linaloripotiwa kubeba pesa hizo, ili kuficha utambulisho wake.

Polisi wameripoti kwamba mshukiwa wa nne, Martin Nderi Nganga alikamatwa katika mtaa wa Kasarani, Nairobi na Ksh9,101,300 zilipatikana katika nyumba yake ya kukodi.

"Pia iliyopatikana ni sanduku la pesa kwenye msitu karibu na Soko la Gataka, katika mtaa wa Karen," NPS ilisema katika taarifa Jumapili asubuhi.

Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia kesi hiyo bado wanaendelea na msako wa kutafuta pesa zilizosalia zilizoibwa na kuwakamata washukiwa wengine zaidi.

Jumatatu jioni, wapelelezi wa makosa ya jinai (DCI) walitoa taarifa kuhusu tukio hilo ambapo walisema wameanzisha msako wa kuwasaka wafanyikazi wawili wa Wells Fargo wanaodaiwa kutoroka na pesa taslimu milioni 94 za Quick Mart.

Daniel Mungai Mugetha ambaye ni kamanda wa kikosi na Anthony Nduiki Waigumu, dereva, waliripotiwa kutoweka na kiasi hicho kikubwa cha pesa baada ya kuliacha gari la kampuni lililokuwa limebeba pesa hizo katika eneo la Dafarm eneo la South C, Nairobi.

DCI waliripoti kuwa washukiwa waliendesha lori hilo kwa siri kutoka kwa afisi ya kampuni hiyo ya ulinzi jijini Nairobi muda mfupi baada ya pesa kupakiwa ndani. Inasemekana waliacha gari la polisi la kusindikiza lililokuwa likisubiri kuruhusiwa kuondoka.

“Bila kujua kwamba lori nambari. KBA 517T walilokuwa wasindikize lilikuwa limeondoka dakika za awali, timu ya wasindikizaji yenye silaha ilikwenda kuuliza kutoka kwa wasimamizi kwa nini upakiaji ulikuwa unachukua muda mrefu sana. Kufikia wakati huo, hakuna lori wala wafanyakazi walioweza kupatikana,” ilisoma ripoti ya DCI.

DCI waliongeza, “Ripoti ya Meneja wa Uchunguzi wa kampuni hiyo ilionyesha kuwa gari hilo aina ya Isuzu Canter lilikuwa likisafirisha pesa kwa benki moja iliyoko mtaa wa Kenyatta Avenue, Nairobi, na lilibeba Sh94 milioni za duka kubwa maarufu nchini.”

Maafisa wa polisi kutoka Lang’ata ambao walihamasishwa kuwatafuta washukiwa hao baadaye walipata lori tupu ambalo lilikuwa na pesa hizo likiwa limetelekezwa katika eneo la South C.

Maafisa wa upelelezi kutoka tawi maalum tangu wakati huo wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta washukiwa na kurejesha pesa zilizoibwa.

DCI pia walitoa picha za washukiwa hao wawili na kuwataka umma kushiriki habari  muhimu zitakazosaidia kukamatwa kwao.