DJ afariki baada ya kuzirai katika ofisi za kituo cha redio

Muhtasari

• Mcheza santuri Alex Nderi almaarufu kama DJ Lithium alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Nairobi baada ya kudaiwa kunywa sumu  kuua panya.

• Kabla ya kuchukua hatua ya kujitoa uhai DJ Lithium pia aliandikia familia na marafiki wake ujumbe akiwafahamisha kwamba ameenda.

Image: HISANI

Hofu ilitanda katika kituo kimoja cha Redio cha hapa nchini usiku wa Jumatano baada ya  mcheza santuri wao mmoja kuzirai ndani ya studio.

Mcheza santuri Alex Nderi almaarufu DJ Lithium alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Nairobi baada ya kuzirai akiwa ofisini.

Duru za kuaminika zimesema kwamba DJ Lithium aliacha kama ameandika barua. Baada ya kuona ameanguka, wafanyikazi wenzake walijitahidi kumwamsha bila mafanikio.

Wafanyakazi wenza wamesema wataachia familia ya mwenda zake  jukumu la kufungua barua ambayo marehemu aliacha. 

DJ huyo anaripotiwa kufuta kurasa zake zote za mitandao ya kijamii kabla ya kuzimia.

Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mkuu wa polisi wa Kilimani Muturi Mbogo amesema Lithium alipelekwa hospitalini kwa ambulans.

"Alithibitishwa kufariki alipofika," alisema.

Kisa hicho kilitokea katika Jumba la Lonroh katikati mwa jiji la Nairobi ingawa polisi walifahamishwa baadaye.

Kulingana na mmoja wa wafanyakazi wenzake, DJ huyo alitaja masuala ya kifamilia kuwa miongoni mwa sababu zilizomfanya achukuwe hatua hiyo.

"Alikuwa na maswala ya kifamilia ambayo alitaja kuwa sababu ya tukio hilo. Tumeshtuka,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.