Serikali ya Kenya, kupitia wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa imesitisha rasmi zoezi la usajili la Sarafu ya Dunia (World Coin) ambalo limekuwa likiendelea katika siku chache zilizopita.
Katika taarifa yake siku ya Jumatano asubuhi, Waziri wa Mambo ya Ndani Kindiki Kithure aliibua wasiwasi wa serikali kuhusu shughuli hiyo yenye utata ambayo imeshuhudia maelfu ya Wakenya wakijitokeza katika maeneo mbalimbali ya usajili wa sarafu hiyo ya kidijitali nchini
Alisema uchunguzi wa uhalali na uhalisi wa mchakato huo umeanza huku shughuli zote zinazohusiana na sarafu hiyo tata zikisitishwa kwa wakati usiobainishwa
"Vyombo husika vya usalama, huduma za kifedha na ulinzi wa data vimeanza uchunguzi ili kubaini ukweli na uhalali wa shughuli hiyo, usalama na ulinzi wa data inayovunwa, na jinsi wavunaji wanavyokusudia kutumia data," Kindiki alisema katika taarifa.
Aliongeza, "Zaidi ya hayo, itakuwa muhimu kwamba uhakikisho wa usalama wa umma na usawa wa shughuli za kifedha zinazohusisha idadi kubwa ya raia utolewe kwa njia ya kuridhisha mapema."
Waziri alisema kuwa serikali imesitisha mara moja shughuli zote za World Coin na mashirika mengine yanayohusika na shughuli kama hiyo nchini Kenya hadi mashirika husika ya umma yatakapothibitisha kutokuwepo kwa hatari zozote kwa umma kwa ujumla.
"Hatua ifaayo itachukuliwa kwa mtu yeyote ambaye anaendeleza, kusaidia, au vinginevyo kujihusisha au kuhusishwa na shughuli zilizoelezwa hapo juu," ilisomeka taarifa hiyo.
Katika siku chache zilizopita, maelfu ya Wakenya wamefika katika vituo mbalimbali vya usajili vya World Coin nchini kote wakitumai kuchuma pesa zilizotajwa kutokana na usajili wa sarafu hiyo ya kidijitali.
Baadhi ya Wakenya waliohojiwa na Radio Jambo wamekiri kupata pesa, wengi wao kati ya shilingi 5000 na shilingi 7000 huku wengine bado wakiwa wameshikilia sarafu za kidijitali walizopewa baada ya kujisajili.