Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza abanduliwa tena

Anakuwa gavana wa kwanza kubanduliwa mara tatu nchini.

Muhtasari

•MCA Kinya alimshutumu Mwangaza kwa makosa matatu: ukiukaji mkubwa wa katiba, utovu wa nidhamu na matumizi mabaya ya ofisi.

•Kinya alisema Mwangaza alitengua uteuzi wa Virginia Kawira kama katibu wa bodi ya utumishi wa umma kaunti hiyo.

GAVANA WA MERU KAWIRA MWANGAZA
Image: EZEKIEL AMING'A

Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ametimuliwa kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka miwili baada ya MCAs kupiga kura kuunga mkono hoja ya yeye kuondolewa madarakani.

Mwangaza alibanduliwa ofisini baada ya MCAs 49 kupiga kura kuunga mkono hoja dhidi ya 17 walioikataa.

Wajumbe watatu walikosa kujitokeza katika mkutano huo wa kura ya kumuondoa madarakani.

Mwangaza atasubiri uamuzi wa Seneti kufahamu iwapo bunge hilo litamwokoa au kuunga mkono kubanduliwa kwake.

Anakuwa gavana wa kwanza kubanduliwa mara tatu nchini.

MCA wa kuteuliwa Zipporah Kinya alimshutumu Mwangaza kwa makosa matatu: ukiukaji mkubwa wa katiba, utovu wa nidhamu na matumizi mabaya ya ofisi.

Katika ukiukwaji mkubwa wa katiba na sheria zingine, Kinya alisema Mwangaza alitengua uteuzi wa Virginia Kawira kama katibu wa bodi ya utumishi wa umma kaunti hiyo.

"Ni bunge la kaunti pekee ndilo lililo na mamlaka ya kubatilisha uteuzi wa katibu wa bodi ya utumishi wa umma katika kaunti," alisema.

Naibu kiongozi huyo alisema Mwangaza alikosa kuwateua Wenyeviti wa Bodi ya Mapato ya Kaunti ya Meru, Meru Microfinance Corporation, Bodi ya Huduma kwa Vijana ya Meru, na Bodi ya Shirika la Uwekezaji na Maendeleo ya Kaunti ya Meru kama inavyotakiwa kisheria hivyo kushindwa kuzifanyia kazi Bodi hizo.

Aliendelea kueleza kuwa Mwangaza alikataa kutekeleza mapendekezo na maazimio ya Bunge la Kaunti yaliyomtaka gavana kuwafuta kazi Katibu wa Kaunti, Kiambi Athiru Thambura, na Mkuu wa Wafanyikazi, Harrison Gatobu Nchamba Mbithi kutoka ofisini kwa ukiukaji mkubwa wa sheria za Katiba. .

Alisema  Kiambi Athiru na mkuu wa wafanyikazi Harrison Gatobu pia wamekuwa wakiwaajiri na kuwafuta kazi kinyume cha sheria lakini Mwangaza hakuchukua hatua yoyote.

Bado katika shtaka hilo la ukiukwaji mkubwa wa katiba na sheria nyingine, Kinya alimshutumu Mwangaza kwa kumfukuza kazi kinyume cha sheria Dk Ntoiti (Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mapato ya Kaunti), Paul Mwaki (Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Vileo), Kenneth Kimathi Mbae (Mkurugenzi Mkuu wa Meru Microfinance Corporation), na Joseph Kithure Mberia (Mkurugenzi Mtendaji, MEWASS) katika unyakuzi wa mamlaka ya mamlaka za uteuzi kinyume na kifungu cha 9 (7)(b) cha Sheria ya Bodi ya Mapato ya Kaunti ya Meru na kifungu cha 10(6) cha Shirika la Uwekezaji na Maendeleo la Kaunti ya Meru.

Kutokana na hatua hiyo, Kinya alisema Serikali ya Kaunti ya Meru imekabiliwa na gharama na fidia ya Sh4 milioni na Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi.