Je, Oparanya kamuidhinisha Malala kuwa gavana wa Kakamega?

Oparanya amedai kuwa ukurasa wake wa Facebook umedukuliwa na chapisho hilo kuwekwa.

Muhtasari

•Oparanya amewasihi Wakenya kupuuza chapisho la hivi punde kwenye ukurasa wake wa Facebook linaloonyesha amemuidhinisha mgombeaji wa ANC Cleophas Malala kwa kiti hicho anachoacha.

•Amebainisha kuwa timu yake tayari imechukua hatua na kuwaomba wanamitandao kutoanguka kwenye mtego wa chapisho hilo.

Gavana Wycliffe Oparanya
Gavana Wycliffe Oparanya
Image: THE STAR

Gavana wa Kakamega anayeondoka Wycliffe Oparanya amewasihi Wakenya kupuuza chapisho la hivi punde kwenye ukurasa wake wa Facebook linaloonyesha kama kwamba amemuidhinisha mgombeaji wa ANC Cleophas Malala kwa kiti hicho anachoacha.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, naibu kiongozi huyo wa ODM amedai kuwa ukurasa wake wa Facebook umedukuliwa na chapisho hilo kuwekwa.

Kufuati hilo, Oparanya amebainisha kuwa timu yake tayari imechukua hatua na kuwaomba wanamitandao kutoanguka kwenye mtego wa chapisho hilo.

"Tunawaomba wanachama na wafuasi wa Azimio la Umoja One Kenya katika Kaunti ya Kakamega wasiwe na hofu na waendelee kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombeaji wa ODM,"  Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano katika ODM ilisoma.

Jumatatu asubuhi, chapisho lilichapishwa kwenye akaunti rasmi ya Facebook ya Oparanya ikiidhinisha Malala wa Kenya Kwanza kuwa gavana wa pili wa kaunti ya Kakamega.

"Pigia kura Cleophas Wakhungu Malalah," Chapisho lililoambatana na picha ya Malala lilisoma.

Maelfu ya wanamitandao ambao walionekana kushangazwa na chapisho hilo walifurika chini yake kutoa maoni yao.

Haya yanajiri huku idadi ndogo ya wapiga kura ikishuhudiwa katika kaunti hiyo huku uchaguzi wa ugavana ukiendelea Jumatatu asubuhi. Zoezi hilo hata hivyo lilikuwa la amani.

Idadi ndogo ya wapiga kura ilishuhudiwa katika vituo vingi vya kupigia kura vya kaunti hiyo ya eneo la Magharibi.

Misururu mirefu iliyoshuhudiwa katika chaguzi za hapo awali katika baadhi ya vituo vya kupigia kura haikuwepo huku wapiga kura wakimiminika katika vituo vya kupigia kura mmoja baada ya mwingine.

Kwa mfano katika kituo cha pili cha Kakamega ACK, wapiga kura 45 pekee kati ya 528 waliojiandikisha kupiga kura walikuwa wamepiga kura kufikia saa nane asubuhi.

Hakukuwa na taarifa za kufeli kwa vifaa vya KIEMS katika kaunti nzima.