Naibu Rais Rigathi Gachagua amewakashifu wakosoaji ambao wameibua masuala kuhusu utumizi wake wa lugha ya Kikuyu katika mikutano ya hadhara.
Akizungumza katika wadi ya Wanjohi, kaunti ya Nyandarua ambapo aliungana na viongozi wa eneo hilo kutoa usaidizi kwa wakazi siku ya Jumamosi, Gachagua alidokeza kuwa baadhi ya 'watu matajiri wa Nairobi ambao hawajapitia shida ' wamekuwa wakimshambulia kwa kutumia lugha ya mama licha ya kwamba sasa ni kiongozi wa kitaifa.
“Wamekuwa wakinikosoa kwa kuongea Kikikuyu. Wanataka niongee kwa Kiingereza, je, mimi ni mzungu?” alihoji.
DP aliweka wazi kuwa hana mpango wa kuacha kutumia lugha ya mama katika majukwaa ya umma ili kuwaridhisha wakosoaji wake, akibainisha kuwa yuko tayari kuacha kiti chake iwapo chaguo lake la lugha litakuwa tatizo.
“Nikija kwenu na kujizuia kuzungumza Kikuyu, nizungumze nini tena? Ikifika mahali nikizungumza Kikuyu nitapoteza kiti hiki, ni sawa ili niendelee kuzungumza lugha yangu,” alisema.
Gachagua alidokeza kuwa yeye ni Mkikuyu kwa kuzaliwa na anajivunia sana lugha yake.
Kiongozi huyo wa pili kwa utawala wa nchi pia alitumia mkutano wa Jumamosi asubuhi kutoa wito wa umoja katika eneo la Mlima Kenya.
Aliwaomba viongozi wa eneo hilo kukumbatia umoja na kuepuka kugawanywa na viongozi kutoka jamii zingine.
"Tupendane, tuwe wamoja na mambo yetu yataendelea kuwa mazuri," alisema.
DP alibainisha kuwa hatawahi kuona aibu kuhusu alikotoka kwani itakuwa nyumbani kwake daima.
"Kamwe sitaona aibu kuwa katika jamii hii kwa sababu hata nikimaliza kazi yangu nitarudi hapa"
Aliendelea kufichua kuwa tayari amepata kipande cha ardhi katika eneo la Ndaragwa ambapo anapanga kujenga ili kuwa karibu na watu wake.
"Mtakuja kunijulia hali, kuniletea malalamishi na baadhi ya bidhaa za shambani," aliwaambia wakazi wa Nyandarua.