Mbunge Oscar Sudi atetea chanzo cha utajiri wake

Sudi, vilevile, alisema anaweza acha siasa kwa muda wa miaka miwili

Muhtasari

• "Nimekuwa nikifanya kazi kabla nikuwe mbunge. Nilinunua Range Rover yangu ya kwanza nikiwa miaka 22. Mnataka tutembee mguu wote?” Alisema Sudi.

• Sudi aliwashangaza wengi baada ya kusema atachukua mapumziko kutoka kwa umma na hataenda katika hafla za umma kutoka kwa wananchi.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Mbunge Oscar Sudi Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Image: MAKTABA

Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, amekana madai kwamba alichanga peke yake shilingi milioni 20 katika hafla ya kanisa ya hivi majuzi.

Katika misururu ya video kwenye jukwaa la X mnamo Juni 30, Sudi alizungumzia madai haya kutoka kwa seneta wa Kakamega Boni  Khalwale ambaye alimshutumu kwa kutoa mchango mkubwa.

Sudi, hata hivyo, aliweka wazi kwamba mchango huo ulikuwa umetoka kwa waumini  wote ambao ulifika shilingi milioni 20 na akasisitiza kuwa haukutoka kwa mtu mmoja ambaye ni yeye jinsi inavyosemekana.

“Inawezekananje wewe unaongea hii uongo mchana? Yaani haumini watu wa kanisa tukiungana tunaweza changa hata Sh50M?” aliuliza Sudi.

“Khalwale na wale wote wananikshifu, Sh20M ilikuwa pesa yote ya mchango. Kanisa ilikuwa imechanga Sh14M. Ya juu tukaongezea mimi na marafiki na watu wengine,” alisema mbunge huyo.

Mbali na hayo, Sudi alieleza chanzo cha utajiri ambako alisema, “ nimekuwa nikifanya kazi kabla nikuwe mbunge. Nilinunua Range Rover yangu ya kwanza nikiwa miaka 22. Mnataka tutembee mguu wote?”

Alitetea mali yake huku akisema kuwa aliyapata kutokana na bidii wala sio mbinu janja.

Maelezo mafupi kwenye video yalisema,”kwa Boni Khalwale, utajiri wangu umepitia bidii isiyo kifani ila wengine wanawaamini washirikina kwa utajiri wa muda mfupi.”

Mbali na hayo, Sudi aliwashangaza wengi baada ya kusema ataenda likizo na hataenda katika hafla za umma kutoka kwa wananchi.

“kuenda mbele, sitashiriki kwenye Harambee kwa kuwa imetumiwa kukashifu na kudharau nia nzuri- wacha ipigwe marufuku. Kwa hivyo, matukio ya sasa kwenye taifa unaita kujichunguza na kwa hivyo, ninachukua likizo ya sabato kutoka kwa shughuli za umma.”

Sudi alieleza makasiriko yake kutokana na chuki na wivu ambao amepata kutoka kwa wanasiasa mbalimbali.

“Nimeenda leave kwa sababu ya kelele na watu weye wivu kama wewe. Watu wengi hawajui vile tunatafuta pesa ya hizi Harambee.”

Vilevile, alisema kuwa anaweza kuacha uanasiasa kwa pamoja. “Mungu akinijalia, akiniongelesha baada ya mwaka mmoja ama miwili nitarudi na nitaanza na hiyo kanisa ya matope ulikuwa unaongelelea,” alimalizia.