•Rengstar anadaiwa kuunda ukurasa wa Facebook kwa jina la Naibu Rais na kuutumia kupata pesa kwa njia ya udanganyifu.
•Mshukiwa alikamatwa katika eneo la Sugoi na wapelelezi wanaofanya kazi katika ofisi ya naibu rais.
Wapelelezi wa DCI wanamzuia mwanamuziki mmoja wa Benga kutoka eneo la Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu kwa madai ya kujifanya naibu rais Rigathi Gachagua.
Collins Kipleting Serem almaarufu Rengstar, 22, anadaiwa kuunda ukurasa wa Facebook kwa jina la Naibu Rais na kuutumia kupata pesa kwa njia ya udanganyifu.
Kulingana na DCI, Rengstar alipata pesa kutoka kwa raia ambao hawakuwa na ufahamu kwa kuwadanganya kuwa walikuwa wakichangia Wakenya wenye njaa.
"Mshukiwa huyo alichapisha nambari ya malipo iliyounganishwa na akaunti katika benki ya Standard Chartered ya Eldoret na kuwasihi wafuasi wake zaidi ya 14K waungane kuchangisha pesa kwa ajili ya waathiriwa wa njaa, akiahidi baraka za Mungu kwa wale ambao wangetii rufaa hiyo," taarifa iliyotolewa na kitengo cha DCI ilisoma.
Mwimbaji huyo kutoka kijiji cha Kamplemur alikamatwa katika eneo la Sugoi na wapelelezi wanaofanya kazi katika ofisi ya naibu rais.
"Kwa sasa mshukiwa yuko chini ya ulinzi akishughulikiwa kwa ajili ya kusomewa mashitaka," walisema DCI.
Haijabainika kiasi cha pesa ambacho mshukiwa alikuwa amefanikiwa kulaghai wafuasi wake kwenye Facebook kabla ya kukamatwa.
Katika mojawapo ya posti ya Rengstar aliyochapisha mnamo Nov 17, mshukiwa anaonekana kuwasihi wasamaria wema kukusanyika pamoja kwa ajili ya Harambee ya umma inayolenga kuchangisha pesa kwa waathiriwa wa ukame.
"Habari za jioni Wakenya, je tukusanye kitu kwa ajili ya Wakenya wenzetu wanaokabiliwa na ukame? Tuungane na kuwafanyia harambee ya umma kwa muda, tubarikiwe sana tunaposaidia," mshukiwa aliandika.
Kufuatia ombi hilo, mshukiwa aliwapa Wakenya akaunti ya kutuma pesa na kuwahakikishia baraka za Mungu.