Msichana wa miaka 16 auawa kwa kuchomwa kisu kufuatia mzozo wa memory card

Mauaji hayo yalitokea nje ya duka la kuuza pombe.

Muhtasari

•Mshukiwa anaripotiwa kuua mwenzake kwa kumdunga kisu kwenye upande wa kushoto wa kifua chake nje ya duka la kuuza vileo la Sweet Wines and Spirit.

•Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa siku za hivi majuzi visa vingi vya utapeli wa simu vimeshuhudiwa katika mji wa Mulot.

Image: TWITTER// DCI

Msichana mwenye umri wa miaka 16 anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mulot, kaunti ya Baringo kwa mauaji ya rafiki yake kufuatia mzozo wa memory card ya 2GB.

Msichana huyo anaripotiwa kuua mwenzake kwa kumdunga kisu kwenye upande wa kushoto wa kifua chake nje ya duka la kuuza vileo la Sweet Wines and Spirits katika kituo cha biashara cha Mulot.

Mwathiriwa ambaye ni rika sawa na mshukiwa alifariki hata kabla ya madaktari katika Hospitali ya Wilaya ya Longisa kujaribu kuokoa maisha yake.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa haijabainika kama wasichana wale ni wanafunzi na walichokuwa wanafanya wasichana wale katika eneo la tukio ambalo ni marufuku kwa watoto.

Polisi kutoka kituo cha Mulot walimtia pingu mshukiwa na kumzuilia huku akisubiri kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka.

Huku hayo yakijiri wapelelezi wanaendeleza uchunguzi zaidi kubaini matukio yaliyozingira kisa hicho cha kuhuzunisha na kuwatia mbaroni wahusika zaidi ikiwa wapo.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa siku za hivi majuzi visa vingi vya utapeli wa simu vimeshuhudiwa katika mji wa Mulot.