logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwili wa mkweaji Cheruiyot Kirui kubaki Mlima Everest, familia yafichua kwa nini

"Cheruiyot alikuwa na mapenzi makubwa kwa milima, na ilimpenda pia.Tunapata faraja kwa kujua anapumzika mahali pake pa furaha," familia ilisema.

image
na Radio Jambo

Habari30 May 2024 - 05:14

Muhtasari


•Familia imefichua uamuzi wa kuuacha mwili ubaki mlimani ulifanywa kufuatia mashauriano ya kina na kuzingatiwa kwa kila hali.

•"Cheruiyot alikuwa na mapenzi makubwa kwa milima, na ilimpenda pia.Tunapata faraja kwa kujua anapumzika mahali pake pa furaha," familia ilisema.

akipumua kwa umbali wa mita 6,000 kwenye Mlima Manaslu, Nepal, mwaka jana.

Familia ya marehemu mpanda mlima wa Kenya Joshua Cheruiyot Kirui imefanya uamuzi mgumu wa kuuacha mwili wake ubaki mahali alipofia kwenye Mlima Everest.

Cheruiyot alifariki Mei 23 alipokuwa akijaribu kukwea kilele cha mlima huo mrefu zaidi duniani bila hewa ya oksijeni ya ziada. Alifariki pamoja na kiongozi wake kwenye safari hiyo, Nawang Sherpa kutoka Nepal.

Familia ya marehemu imefichua kuwa uamuzi wa kuuacha mwili wake ubaki mlimani ulifanywa kufuatia mashauriano ya kina na kuzingatiwa kwa kila hali.

"Cheruiyot alianguka kwenye shimo lililo umbali wa mita 48 kutoka kwenye kilele (mita 8,848) na kurejesha mwili wake kutoka juu itakuwa hatari kwa timu ya uokoaji," familia ya Cheruiyot ilisema katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano.

Waliongeza, “Familia haitaki kuhatarisha maisha yoyote. Cheruiyot alikuwa na mapenzi makubwa kwa milima, na ilimpenda pia. Tunapata faraja kwa kujua anapumzika mahali pake pa furaha.

Familia ya marehemu mpanda milima huyo ilitoa shukrani za dhati kwa upendo na sapoti ambayo wamepokea kutoka kote ulimwenguni tangu tukio hilo la bahati mbaya kutokea.

Pia waliifariji familia ya marehemu Nawang Sherpa aliyefariki pamoja na marehemu Cheruiyot.

“Kutakuwa na ibada ya ukumbusho jijini Nairobi na katika kijiji cha Chepterit, taarifa kuhusu hili itawasilishwa kwa wakati ufaao. Usaidizi kwa familia unaweza kutumwa kupitia; Paybill: 522533, Account: 9229224, Name: Cheruiyot Kirui Fundraising,” familia hiyo ilisema.

Siku ya Ijumaa wiki iliyopita, familia ya marehemu Cheruiyot ilieleza masikitiko yao kufuatia kufariki kwa mmoja wao.

Walithibitisha kwamba marehemu pamoja na muongozi wake Nawang Sherpa walipoteza mawasiliano na kambi ya chini kabla ya wote wawili kuanguka.

"Sote tumehuzunishwa na yaliyompata ndugu yetu Cheruiyot Kirui kwenye Mlima Everest," familia ya Cheruiyot ilisema kwenye taarifa.

"Cheruiyot alipoteza mawasiliano ya redio na kambi yake mapema asubuhi ya Mei 22, 2024 katika harakati zake za kukwea hadi kilele. Aliripotiwa kutoweka na mwenzake katika msafara na mara moja timu ya waokoaji waliokuwa kwenye kambi ya 4 walitumwa hadi kufikia hatua ya kuwasiliana mara ya mwisho.

Mwili wake uligunduliwa kwenye mwinuko wa mita 8,800, mita 48 kutoka kwenye kilele. Ingawa haiwezekani kubainisha matukio yaliyojiri kikamilifu, tunajua kwamba Cheruiyot na muongozi wake wa sherpa, Nawang Sherpa, walianguka,” taarifa hiyo ilisoma zaidi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved