Naibu gavana wa Kakamega awakashifu walimu kwa kuwaagiza wanafunzi kuleta kuku shuleni

Savula ametaka mtaala wa CBC kutupiliwa mbali huku akisema kuwa hauwezi kufanya kazi nchini Kenya.

Muhtasari

•Savula aliwashtumu walimu kwa  kuwatuma wanafunzi nyumbani kuchukua kuku kwa ajili ya matumizi katika masomo ya CBC.

•Baada ya kuapishwa kwake, Rais William Ruto aliahidi kuangaliwa upya kwa CBC ili kuwapa wazazi njia bora zaidi.

Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula
Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula
Image: MAKTABA

Wanasiasa mbalimbali wameendelea kuukosoa mfumo wa elimu wa CBC ambao ulianzishwa hapa nchini miaka mitano iliyopita.

Naibu gavana wa kaunti ya Kakamega Ayub Savula ametaka mtaala huo utupiliwe mbali huku akisema  kuwa hauwezi kufanya kazi katika nchi ambayo asilimia kubwa ya watu wanaishi maisha hohehahe.

Katika taarifa yake ya Jumamosi, Savula aliwashtumu walimu kwa  kuwatuma wanafunzi nyumbani kuchukua kuku kwa ajili ya matumizi katika masomo ya CBC.

"Nilidhani ni uvumi tu hadi nilipojionea mwenyewe. Walimu wakiwatuma wanafunzi nyumbani si kwa ada, bali kuleta kuku kwa jina la mtaala wa CBC," Savula alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Aliongeza, "CBC hii lazima ikomeshwe. Haiwezi kufanya kazi katika nchi ambayo nusu ya watu wetu pekee wanaweza kuweka chakula cha heshima mezani,"

Savula anajiunga na orodha kubwa ya wanasiasa ambao wameagiza kutupiliwa mbali kwa mtaala wa CBC.

Mnamo Ijumaa Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa aliwashutumu walimu kwa kuwadhulumu wazazi kupitia  mtaala wa CBC..

Barasa alidai kuwa walimu wamekuwa wakiwaagiza wanafunzi kubeba kuku shuleni kwa ajili ya masomo ila badala yake wanazitumia kama chakula majumbani mwao.

"Walimu wamekula kuku mpaka imeisha kwa boma la watu, hio CBC tunataka iondolewe kabisa," alisema.

Alibainisha kuwa Rais William Ruto anafaa kutupilia mbali mtaala wa CBC akisema unajitokeza kuwa mzigo kwa wazazi Wakenya.

Baada ya kuapishwa kwake, Rais William Ruto aliahidi kuangaliwa upya kwa CBC ili kuwapa wazazi njia bora zaidi.

Alisema atateua jopo la marekebisho ya elimu katika wiki zijazo ili kutoa ushauri juu ya njia ya kusonga mbele.

"Litakusanya maoni kutoka kwa wahusika wote muhimu kulingana na matakwa ya kikatiba ya ushiriki wa umma," Rais alisema.

"Ninafahamu wasiwasi juu ya mabadiliko pacha ya darasa la mwisho la 8-4-4 na darasa la kwanza la CBC mnamo Januari mwaka ujao. Ninawahakikishia kutakuwa na suluhu ya suala hilo kabla ya wakati huo.” alisema.