"Nimezizoea!" Sudi awajibu wanaomkosoa kwa kuabiri ndege ya Kenya Air Force

"Nimezoea helikopta hizi za serikali. Picha hizi zinaonyesha nilipokuwa na uhuru na wakati sikuwa nao," aliandika

Muhtasari

•Ijumaa jioni mbunge huyo alichapisha picha za safari za safari zake za awali kwenye helikopta za serikali.

•Seneta wa Narok Ledama Olekina alisema kuwa hatua ya mbunge wa Kapseret ni ubadhirifu wa pesa za umma.

akitoka kwenye ndege ya Kenya Airforce huko Naivasha, kaunti ya Nakuru mnamo Ijumaa, Septemba 16, 2022
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi . akitoka kwenye ndege ya Kenya Airforce huko Naivasha, kaunti ya Nakuru mnamo Ijumaa, Septemba 16, 2022
Image: HISANI

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amekashifu watu wanaokosoa hatua yake ya kuabiri ndege ya Kenya Airforce kuhudhuria mkutano wa  Wabunge wa Kenya Kwanza mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.

Ijumaa jioni mbunge huyo alichapisha picha za safari za safari zake za awali kwenye helikopta za serikali.

"Nimezoea helikopta hizi za serikali. Picha hapa chini zinaonyesha nilipokuwa na uhuru na wakati sikuwa nao," aliandika chini ya picha hizo.

Mbunge huyo wa muhula wa tatu alitoa taarifa hiyo baada ya mazunhumzo makubwa kuzuka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hatua yake kutumia ndege ya serikali.

Baadhi ya Wakenya akiwemo wanasiasa maarufu walistaajabu kumuona mbunge huyo akifurahia safari ya Kenya Air Force huku baadhi wakihoji kama alistahili kufanya hivyo.

Seneta wa kaunti ya Narok Ledama Olekina alisema kuwa hatua ya mbunge wa Kapseret ni ubadhirifu wa pesa za umma.

Ledama alihoji iwapo Sudi ndiye waziri mpya wa Ulinzi katika serikali ya rais William Ruto.

"Je, huyu ni Waziri mpya wa Ulinzi? Ni ufujaji ulioje wa rasilimali za umma .... Bottom Up my foot!" alisema kupitia Twitter.

Kwa kawaida, chopa za kijeshi zinahifadhiwa Rais, Naibu rais, maafisa wakuu wa kijeshi na mawaziri wa Mambo ya Ndani na Ulinzi.