Probox iliyokuwa ikisafirisha nyama ya punda hadi Nairobi yaanguka vibaya Mai Mahiu

Mwanaume mmoja alijeruhiwa katika ajali hiyo ya Jumanne asubuhi na kukimbizwa katika hospitali ya Tigoni.

Muhtasari

•Gari hilo lilianguka baada ya kupoteza mwelekeo na kuondoka barabarani katika eneo la Kotoka Mai Mahiu, Kaunti ya Kiambu.

•Shahidi alidokeza kuwa kumekuwa na mashaka ya biashara ya nyama ya punda huku baadhi ya wakazi wakiripoti kupotea kwa punda wao.

Image: MAKTABA

Gari ambalo lilikuwa likisafirisha nyama inayoaminika kuwa ya punda lilianguka vibaya baada ya kupoteza mwelekeo na kuondoka barabarani katika eneo la Kotoka Mai Mahiu, Kaunti ya Kiambu.

Mwanamume anayeshukiwa kuwa dereva wa gari hilo aina la Probox alijeruhiwa katika ajali hiyo ya Jumanne asubuhi na kukimbizwa katika hospitali ya Tigoni.

Bosi wa polisi aliyezungumza na Citizen Digital alisema mshukiwa ambaye anaendelea kupokea matibabu chini ya uangalizi wa polisi baadaye atafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kusafirisha nyama ambayo haijakaguliwa inayoshukiwa kuwa ya punda.

“Gari hilo lilikuwa likisafiri kuelekea Nairobi ikapata ajali. Ni ajali iliyojisababishia yenyewe ambapo ilibingiria barabarani na kumjeruhi mtu mmoja ambaye tunashuku kuwa dereva, na ambaye sasa amelazwa katika hospitali ya Tigoni akilindwa huku uchunguzi ukiendelea,” afisa huyo alisema.

Shahidi aliyezungumza na kituo hicho alisema alikimbia katika eneo la tukio na ndani ya gari hilo lililoharibika akaona nyama ambayo baada ya kuitazama vizuri aligundua kuwa ni ya punda.

Aidha alidokeza kuwa kumekuwa na mashaka ya biashara ya nyama ya punda huku baadhi ya wakazi wakiripoti kupotea kwa punda wao na wengine kupata mifupa iliyotapakaa.

“Watu wamekuwa wakiteta kwa sababu ata kuna mahali unakuta mifupa na nini. Sasa tunaona biashara na wengine wamelalamika punda wa wamekuwa wakiibiwa,” shahidi huyo alisema.

Shahidi mwingine miongoni mwa watu wa kwanza kufika eneo la tukio alisema hawana uhakika ni watu wangapi waliokuwa kwenye gari hilo.