Raila na Ruto watoa Sh800,000 kwa waathiriwa wa moto Machakos

Muhtasari

•Raila alituma mchango wa Sh500,000 huku Ruto akichangia Sh300,000 kusaidia waathiriwa hao.

•Muthama aliwapa wafanyabiashara hao Sh20,000 kwa ajili ya kufungua akaunti maalum ya benki.

•Maliti alisema kaunti ilituma washauri katika eneo la tukio ili kuchukua data na kutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa.

Wafanyabiashara wakichukua baadhi ya bidhaa zao zilizoteketea kutoka kwa majengo yaliyoteketezwa katika soko la Gregon mjini Machakos mnamo Jumanne, Juni 7.
Wafanyabiashara wakichukua baadhi ya bidhaa zao zilizoteketea kutoka kwa majengo yaliyoteketezwa katika soko la Gregon mjini Machakos mnamo Jumanne, Juni 7.
Image: GEORGE OWITI

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga na mwenzake wa Kenya Kwanza Naibu Rais William Ruto wametoa jumla ya Sh800,000 kwa waathiriwa wa moto katika kaunti ya Machakos.

Raila alituma mchango wa Sh500,000 huku Ruto akichangia Sh300,000 kusaidia waathiriwa hao.

Spika wa bunge la kaunti ya Machakos Florence Mwangangi alisema Raila alimtuma na mchango wa laki tano kuwasilisha kwa waathiriwa kupitia uongozi wa Muungano wa Masaku Juakali.

Mwangangi ndiye mgombea mwenza wa Nzioka Waita katika kinyang'anyiro cha ugavana Machakos. Waita ni mkuu wa zamani wa wafanyikazi wa Ikulu. Wanagombea kwa tiketi ya CCU ambapo Waita ndiye kiongozi wa chama.

Alisema yeye na Waita na watachangia Sh700,000 kwa ajili hiyo hiyo.

Mwangangi alizungumza alipowatembelea wafanyabiashara katika soko la Grogon mjini Machakos siku ya Jumanne. Moto huo uliodumu kwa zaidi ya saa nane uliharibu miundo kadhaa ya biashara, na kuathiri wafanyabiashara zaidi ya 500.

Mwenyekiti wa kitaifa wa UDA Johnson Muthama na Mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka walitembelea wafanyabiashara hao.

Muthama alitoa Sh520,000, mchango wake wa kibinafsi na kusema Ruto aliahidi Sh300,000 kwa wafanyabiashara huku Munyaka akitoa Sh100,000.

Muthama aliwapa wafanyabiashara hao Sh20,000 kwa ajili ya kufungua akaunti maalum ya benki ili kuchangisha fedha kwa ajili ya waathiriwa hao. Alijitolea kuwa mwenyekiti wa mfuko wa fedha.

Aliwaambia wafanyabiashara hao kupitia kwa mwenyekiti wa muungano huo Mumo Kilonzo kuharakisha mchakato wa kufungua akaunti ya benki ili wapitishe pesa hizo kwenye akaunti.

Viongozi hao walilaumu moto huo kwa kile walichokitaja kuwa ulegevu kwa upande wa serikali ya kaunti ya Machakos.

Walisema kuwa utawala wa Gavana Alfred Mutua hauna uwezo wa kujibu huduma za dharura kama vile moto.

Hata hivyo, Naibu Gavana wa Machakos, Francis Maliti, katika muunganisho wa haraka, alipinga madai hayo, akisema utawala wao unawajibika na uwezo wa kushughulikia kila aina ya dharura, ikiwa ni pamoja na milipuko ya moto kote nchini.

Maliti alisema kaunti ilituma washauri katika eneo la tukio na kuweka dawati la ushauri nasaha kuchukua data na kutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa kutokana na kiwewe kilichowakumba.

"Ni hali ya kusikitisha kwa sababu mali nyingi ziliharibiwa. Tuligundua mashine nyingi za gharama iliyoteketezwa. Gari moja la zima moto la serikali ya kaunti ya Machakos halikuweza kuudhibiti moto huo,” Mwangangi alisema.

"Bunge la kaunti kila mara limekuwa likitekeleza wajibu wake kuhakikisha kuwa sheria, sera na bajeti zinazofaa zinapitishwa ili maafa ya aina hii yakitokea, yasizidi."

Aliongeza kuwa kama bunge, walikuwa na matatizo ya utekelezaji wa sheria, bajeti na sera zilizopitishwa, hasa na ofisi ya gavana.

“Mwaka 2021 tulipitisha sheria iliyopendekeza kuwekwa hazina ya dharura. Bunge lilikuwa likichochea sheria hiyo kwa muda," alisema.

 "Tulimuita Maliti ambaye alikuwa msimamizi wa hati ya fedha ya kaunti, na ilikuwa ni vuta nikuvute hadi tukafaulu kupitisha sheria. Maliti na Mutua wanapaswa kutuambia ni nini kiliwekwa kwenye hazina hiyo." 

Alisema uharibifu haungekuwa mkubwa kama ulivyokuwa ikiwa mfuko huo ungetumika ipasavyo. 

"Tulipata mchango kutoka kwa mmoja wa wafanyabiashara mashuhuri katika mji huu, Bw Theuri wa Pasha Enterprises, ambaye alitoa Sh50,000 huku aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa Machakos Susan Musyoka akichangia Sh10,000," Mwangangi alisema. 

“Bado tunawashawishi marafiki wengine, taasisi za serikali na washirika wengine. Ni lazima tuhakikishe wanarejea kwa sababu wanapigwa lakini hawajashindwa.”

(Utafsiri: Samuel Maina)