"Sina damu mikononi mwangu!" Rais Ruto avunja kimya kuhusu mauaji ya waandamanaji

Rais amejaribu kujisafisha kutokana na makosa yoyote kufuatia mauaji ya zaidi ya watu 20 wakati wa maandamano.

Muhtasari

•Rais alisisitiza kuwa ni watu 19 pekee waliopoteza maisha, na sio 24 jinsi inavyodaiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

•Ruto alisema mali ya thamani ya Sh2.4 bilioni iliharibiwa au kuteketezwa wakati wa maandamano.

akizungumza wakati wa mahojiano ya Jumapili, Juni 30, 2024, katika ikulu ya Nairobi.
Rais William Ruto akizungumza wakati wa mahojiano ya Jumapili, Juni 30, 2024, katika ikulu ya Nairobi.
Image: HISANI

Rais William Ruto amejaribu kujisafisha kutokana na makosa yoyote kufuatia mauaji ya zaidi ya watu 20 wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Akizungumza wakati wa mazungumzo na wanahabari kutoka Ikulu ya Nairobi, rais alisisitiza kuwa ni watu 19 pekee waliopoteza maisha, na sio 24 jinsi inavyodaiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Alisema ametimiza ahadi yake kwamba hakutakuwa na mauaji ya kiholela nchini Kenya.

"Sina damu mikononi mwangu. Watu 19 wako kwenye rekodi kwamba wamekufa. Bahati mbaya sana, kama demokrasia, hiyo haifai kuwa sehemu ya mazungumzo yetu," Ruto alisema alipoulizwa maoni yake kuhusu maisha ambayo imepotea.

Hata hivyo, alitaja vifo hivyo kuwa vya bahati mbaya akisema havipaswi kutokea katika demokrasia.

Ruto alisema mali ya thamani ya Sh2.4 bilioni iliharibiwa au kuteketezwa wakati wa maandamano yaliyotokea katika wiki mbili zilizopita.

Alipoulizwa jinsi alivyohisi kuhusu kifo cha mvulana wa umri wa miaka 12 katika mtaa wa Rongai, Ruto alisema maisha yoyote yanayopotea lazima yasumbue kila mtu, akiwemo yeye.

"Nitampa mama wa mtoto huyo wa miaka 12 maelezo ya kile kilichotokea na kuhakikisha kwamba tunaleta hali ambayo kama mimi ambaye nina watoto, mtoto wake anaweza kuhesabiwa," alisema.

Rais alishikilia kuwa wahalifu walichukua fursa ya maandamano kuharibu mali na kuchoma Bunge na miundombinu mingine muhimu ya serikali.