Utata huku Padre wa Katoliki akifariki baada ya kuburudika usiku kucha na mpenzi wake Murang'a

Padre Joseph Kariuki na mpenzi wake walikaa hotelini usiku kucha kabla ya yeye kuugua asubuhi iliyofuata.

Muhtasari

•Padre Joseph Kariuki Wanjiru mwenye umri wa miaka 43 alikuwa pamoja na mwanamke anayedaiwa kuwa mpenzi wake.

•Inasemekana kasisi huyo alikula kuku na akabugia kileo siku ya Ijumaa usiku kabla ya kulala katika hoteli hiyo.

Padre Joseph Kariuki
Image: HISANI

Polisi katika Kaunti ya Murang’a wanachunguza kisa ambapo Padri wa Kanisa Katoliki alifariki katika chumba cha hoteli katika kaunti ndogo ya Gatanga siku ya Jumamosi asubuhi.

Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Gatanga Lawrence Njeru, Joseph Kariuki Wanjiru mwenye umri wa miaka 43 alikuwa pamoja na mwanamke anayedaiwa kuwa mpenzi wake.

Walikaa hotelini usiku kucha kabla ya yeye kuugua asubuhi iliyofuata.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32 anasemekana kuwa mfanyakazi katika kanisa moja analotumikia kasisi huyo.

Inasemekana kasisi huyo alikula kuku na akabugia kileo siku ya Ijumaa usiku kabla ya kulala katika hoteli hiyo.

Wafanyikazi wa hoteli hiyo walisema alikuwa mteja katika hoteli hiyo kwa miaka miwili iliyopita.

Baada ya tukio hilo kutokea, inasemekana mwanamke huyo aliwataarifu wasimamizi wa hoteli hiyo kuwa kasisi huyo alikuwa mgonjwa na alikuwa akisumbuliwa na kizunguzungu.

Walimfunika blanketi na kumweka nyuma ya gari lake aina ya Toyota Harrier na kumkimbiza katika hospitali ya Kenol ambako alifikwa na mauti.

Mwanamke huyo ambaye alikuwa ameandamana na wafanyikazi kadhaa wa hoteli hiyo kisha alielekea kituo cha polisi cha Samuru ambapo waliwaarifu polisi kuhusu tukio hilo kabla ya kurekodi taarifa.

Njeru alisema walipata mwili wa marehemu nyuma ya gari, nusu ukiwa umefunikwa na blanketi.

“Mwili ulikuwa safi lakini povu lilikuwa likitoka mdomoni. Tulifanya uchunguzi na kugundua kwamba miili ya makasisi haiwezi kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha kawaida kwa hivyo tulifanya mipango ya kusafirishwa hadi Nairobi, tukiandamana na maafisa wetu”.

Njeru hata hivyo alibainisha kuwa uchunguzi umeanza kubaini chanzo cha kifo chake.

"Tulimhoji aliyekuwa ameandamana naye w na akatuambia alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kasisi kwa miaka sita iliyopita," mkuu wa polisi alisema zaidi.