Video ya kutisha yaonyesha jinsi majambazi waliojihami walivyomwibia mwanamke Rongai

Muhtasari

•Katika video hiyo ya kuogofya, mhasiriwa aliviziwa na genge la takriban majambazi sita alipokuwa akiingia kwenye boma lake.

•Mwanamke huyo anaonekana akijaribu kutoroka lakini alikuwa amezidiwa na idadi ya wavamizi wake.

Picha ya skrini ya CCTV ya wizi huo mnamo Jumapili, Juni 12, 2022
Picha ya skrini ya CCTV ya wizi huo mnamo Jumapili, Juni 12, 2022
Image: HISANI

Mwanamke mmoja aliibiwa Jumapili usiku huku akiwa amenyooshewa bunduki nyumbani kwake katika eneo la Gataka, Ongata Rongai.

Video za CCTV zilizopakiwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha kwamba wizi huo wa ulitekelezwa ulitokea mwendo wa saa nane na dakika ishirini usiku. 

Katika video hiyo ya kuogofya, mhasiriwa aliviziwa na genge la takriban majambazi sita alipokuwa akiingia kwenye boma lake.

Jambazi mmoja anaonekana akikimbia kwenye mlango wa dereva na kumyoonyeshea mhasiriwa bunduki huku akimwagiza afungue kabla ya kumuita mmoja wa washirika wake.

Jambazi wa pili anaoneka akijaribu kuvunja dirisha la upande wa abiria kwa panga bila mafanikio. Kisha anapitisha panga hiyo kwa jambazi wa kwanza aliyekuwa na bunduki  ambaye anafanikiwa kuvunja  dirisha la dereva kwa majaribio tano.

Wakati huo, jambazi mwingine zaidi anatoka kwenye maegesho ya magari huku mwingine akiingia ndani ya boma hilo kutoka nje akiwa amebeba kile kinachoonekana kama bunduki aina ya AK 47.

Mwanamke huyo anaonekana akijaribu kutoroka lakini alikuwa amezidiwa na idadi ya wavamizi wake.

Kisha ugomvi unatokea kati ya mhasiriwa na jambazi aliyeshika bastola katika jaribio la  kumfanya afungue mlango. Hatimaye anakubali kufungua mlango baada ya jambazi huyo kumtishia mara kadhaa.

Mhasiriwa kisha anatolewa nje ya gari huku wanne hao wakianza kupekua gari kwa ajili ya vitu vya thamani.

Katika hatua hii, jambazi wa tano anaingia kwenye kiwanja huku akiwa amebeba tochi. Muda mfupi baadaye, jambazi wa sita anamfuata huku jambazi mwenye bunduki ya AK 47 akimvuta mwanamke kuelekea kwa nyumba yake.

Mhasiriwa anaonekana akijaribu kujadiliana na majambazi bila mafanikio.

Tukio hilo lilichukua wastani wa dakika mbili.

Video ya pili ya CCTV inayonasa sebule ya nyumba ilianza mwendo wa saa nane na dakika 22 usiku. 

Mwanamke huyo anaongozwa ndani ya nyumba yake na jambazi mwenye bunduki aliyekuwa amevalia kofia.

Mmoja wa majambazi anaingia ndani ya vyumba vingine huku jambazi mwingine akipora stendi ya runinga kutafuta vitu vya thamani.

Wakati huu wote, mwanamume aliyevalia kofia anaendelea kumtesa mhasiriwa kabla ya mwenzake kwenye stendi ya runinga kumshika, kumsukuma kwenye kochi na kuonekana kumpiga kofi kabla ya kuvua viatu vyake miguuni mwake.

Majambazi wengine wawili kisha wanaonekana wakiingia ndani ya nyumba, mmoja akiwa amebeba tochi.

Jambazi mwenye kofia kisha anamvuta mwanamke huyo kwa miguu yake na kuanza kumtishia kwa bunduki huku wengine wakimsukuma kuelekea chumbani.

Picha hiyo ya dakika 2:04 inaisha huku majambazi wakiendelea kupora nyumba huku wakipakia vitu vya thamani kwenye begi.