Waziri Moses Kuria avunja kimya baada ya China Square kufunguliwa tena

Kuria alisema kufunguliwa tena kwa China Square ni njama ya watu wa tabaka la kati.

Muhtasari

•Akizungumza siku ya Jumatano, Kuria alisema kuwa China Square ni ya watu wa tabaka la kati nchini.

•Waziri huyo alisema ana wajibu kwa Watu kumtazama kama Waziri ili kuwapa mwelekeo ambao nchi inapaswa kuchukua.

Waziri wa Biashara Moses Kuria
Image: MAKTABA

Waziri wa Biashara Moses Kuria amesema ana wajibu wa kuzungumza kwa niaba ya wafanyibiashara na watengenezaji wa bidhaa nchini Kenya baada ya China Square kufunguliwa tena.

Akizungumza siku ya Jumatano, Kuria alisema kuwa China Square ni ya watu wa tabaka la kati nchini.

"Hii China Square. Je, kuna kituo cha matatu pale, hakuna? Kwa hiyo ni nani anafanya ununuzi kwenye China Square? Hawa ni watu wanaoendesha magari; tabaka la kati la nchi hii," alisema.

"Huyo mtu wa tabaka la kati ambaye anafanya manunuzi huko amewalipia karo watoto wake, lakini yule mchuuzi halisi wa Dandora anayehangaika kuuza samaki hajui mlo unaofuata utatoka wapi."

Aliongeza kuwa kufunguliwa tena kwa China Square ni njama ya watu wa tabaka la kati.

Waziri huyo alisema ana wajibu kwa Watu kumtazama kama Waziri ili kuwapa mwelekeo ambao nchi inapaswa kuchukua.

Kuria alisema kuwa watengeza bidhaa na wafanyibiashara wa humu nchini Kenya wanasaidia uchumi licha ya wao kutokuwa na sauti kwenye mitandao ya kijamii.

"Hustlers hawapo kwenye Twitter au TikTok, hawawezi kunukuliwa kwenye TV, huku baadhi ya wanaume wa tabaka la kati nchini wanapiga kelele mtandaoni," alisema.

"Hii haisaidii nchi yetu. Nina wajibu wa kumzungumzia mfanyibiashara wa Gikomba na Kamukunji ambaye hana sauti kwenye Twitter."

Matamshi ya Waziri huyo yanakuja siku chache baada ya China Square kufungua tena milango yake baada ya kufungwa kwa muda kutokana na mzozo na Kuria.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu na Chama cha Wafanyibiashara wa China, mazungumzo kadhaa na serikali ya Kenya yamefanywa ili kuruhusu China Square kuendelea kufanya kazi nchini Kenya.

"Chama cha Wafanyabiashara wa Kichina cha Kenya kinakaribisha habari njema za kuanzishwa tena kwa shughuli za uwanja wa China Square kufuatia mazungumzo kadhaa kati ya Serikali ya Kenya na Jumuiya ya Wachina nchini Kenya kutafuta suluhu la mzozo," ilisema taarifa hiyo.

"Chemba inatazamia kutendewa kwa usawa na haki kwa biashara zote katika bodi ili kuhakikisha mazingira mazuri ya biashara kwa wote na kukuza uhusiano mzuri kwa msingi wa kuaminiana na kufaidika."

Watu wananitazama ili niwape mwelekeo ambao nchi inapaswa kuchukua.