Unai Emery awapa wanabunduki uhuru wa kuchagua nahodha wanayemtaka

Unai Emery aliwauliza wachezaji wa Arsenal kumpigia kura nahodha waliyemtaka, mlinzi Rob Holding amefuchua.

Emery alitoa orodha ya wachezaji watano alipoteuliwa msimu uliopita wa joto lakini wachezaji hao wakapungua kufuatia kuondoka kwa Laurent Koscielny, Petr Cech na Aaron Ramsey.

Granit Xhaka ameteuliwa kama nahodha msimu huu wa ligi ya Premier lakini alizomewa juzi na mashabiki waliposhinda dhidi ya Aston Villa huku Mesut Ozil akiwa mchezaji aliyesalia kutoka orodha ya awali.

Mauricio Pochettino amewahakikishia mashabiki wa Tottenham kwamba amejitolea kikamilifu kubadilisha msimu wao. Spurs wameshinda mechi mbili tu kati ya nane za ufunguzi kwenye mashindano yote msimu huu, na walibanduliwa nje ya kombe la Carabao Cup jumanne.

Tayari wako alama 10 nyuma ya viongozi wa ligi ya Primia Liverpool na Pochettino anakiri kwamba jambo hilo linamuumiza. Watachuana na Southampton Jumamosi kabla ya kutembelewa na Bayern Munich katika mechi ya ligi ya mabingwa Jumanne ijayo.

West Ham wanawania kumsajili mshambulizi wa Croatia Mario Mandzukic katika kipindi kifupi cha uhamisho mwezi Januari. Mandzukic amekua akichezeshwa kama akiba msimu huu tangu kocha Maurizio Sarri, kujiunga na Juve, na alikua anawindwa na United mwanzoni wa msimu huu  lakini mazungumzo yalitubuka.

Klabu ya Qatari Al-Rayyan ilimpa ofa ya pauni million saba kwa mwaka lakini alikataa, kwani anataka kucheza katika ligi ya Uingereza.

Nahodha wa Bandari Felly Mulumba anaamini wakizuia ngome vizuri dhidi ya Ben Guerdane ya Tunisia Jumapili, watapata angalau sare na kufuzu kwa awamu ya makundi katika kombe la mashirikisho ya bara Afrika.

Bandari ambao waliwasili Tunis leo, wanaongoza 2-0 katika mkondo wa kwanza uliochezwa jijini Nairobi, na wanahitaji sare ili kuandikisha historia.

Timu hio imepigwa jeki kwa kurejea kwa kiungo Abdalla Hassan ambaye alikua amejeruhiwa.

Bingwa wa  Olimpiki, wa mbio za  Commonwealth za mita 1,500 Faith Kipyegon anaamini yuko katika hali dhabiti, kabla ya kuanza kwa mbio za ubingwa wa dunia leo jijini Doha, Qatar.

Kipyegon ambaye atakua akitetea taji lake alikosa msimu wote wa mwaka 2018 kutokana na likizo ya baada ya kujifungua. Huku mpinzani wake wa jadi Genzebe Dibaba wa Ethiopia akikosa mbio hizo kutokana na jeraha Kipyegon na Sifan Hassan wa Uholanzi wanapigiwa upatu kunyakua medali.