Sofapaka wapata afueni baada ya kupata ufadhili wa milioni 35

Sofapaka wamepata afueni ya masaibu ya kifedha yanayokumba soka humu nchini, baada ya kampuni ya kamari Betika kutangaza ufadhili upya wa klabu hiyo wa shilingi milioni 35 kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kiwango hiki ni zaidi ya cha mwaka uliopita ambacho kilikua shilingi milioni 15, na mkuu wa biashara wa kampuni hio John Mbatia, anasema misheni yao ni kuunga mkono spoti humu nchini.

Afrika Kusini itakua nchi ya mwisho kuwasili humu nchini kwa kipute cha raga cha Safari Sevens wikendi hii katika uwanja wa RFUEA.

The Blitz Bokke wanatarajiwa kuwasili kesho saa kumi na moja asubuhi. Wataongozwa na gwiji wa raga Cecil Afrika ambaye anaregea kwenye ikosi hicho baada ya kukosa msimu uliopita kutokana na majeraha.

Mabingwa hao wa dunia wa zamani wako katika kundi A pamoja na Kenya Morans, Uganda na Burundi. Jumla ya timu 16 zitashiriki kipute hicho.

Tukielekea ulaya, Paul Pogba na David de Gea watakosa mechi ya Manchester United ya Super Sunday dhidi ya  Liverpool kutokana na majeraha.

De Gea alilazimika kuondoka uwanjani wakati wa mechi ya Uhispania ya kufuzu kwa Uro dhidi ya Uswidi jumanne akiwa na jeraha la mguu. Kukosekana kwa De Gea kuna maana kua Sergio Romero atacheza katika ikosi cha kwanza msimu huu.

De Gea anajiunga na Paul Pogba na Jesse Lingard ambao pia hawatacheza.

La Liga inataka mechi ya El Clasico ya tarehe 26 mwezi huu ichezwe Bernabeu kwa Real Madrid badala ya Nou Camp kwa Barcelona kutokana na hofu ya kutokea machafuko ya kiraia.

Kumekua na maandamano Barcelona baada ya viongozi 9 wa Catalan kukamatwa siku ya jumatatu. La Liga iliwasilisha ombi hilo kwa shirikisho la soka nchini Uhispania na vilabu vyote viwili vitaulizwa maoni yao.

Barcelona na Real Madrid hawakuhusika na ombi la La Liga la kwanza na hakujakua na taarifa zozote kutoka kwa vilabu hivyo.