Hatuna pesa za kuipeleka Harambee Stars Misri - Nick Mwendwa

FKF imekiri kuwa haina pesa ya kuwapeleka Harambee Stars kwa kipute cha wiki ijayo cha kufuzu kwa AFCON nchini Misri.

Rais Nick Mwendwa anasema hawajapokea majibu yoyote kutoka kwa serikali, kuhusiana na ombi lao la ufadhili. Mwendwa anaonya kuwa Kenya itaadhibiwa iwapo itakosa mechi hiyo, ikiwemo kupigwa marufuku ya michuano ya kufuzu kwa AFCON mwaka wa 2023.

Pia ameteta kwamba hakuna tikiti zimetolewa kwa Harambee Starlets kabla ya mechi yao ya kufuzu kwa Olimpiki ya Tokyo mwaka 2020 dhidi ya Zambia wiki ijayo.

Nairobi City Stars waliendeleza mchezo mzuri katika National Super League baada ya kuwafunga Migori Youths 2-1 ugani Camp Toyoyo.

Mabao ya Wycliffe Otieno na Oliver Maloba yalitosha kumpa kocha Sanjin Alagi ushindi wake wa 10 msimu huu na kusalia kileleni wakiwa na alama 32. Nahodha Calvins Masawa anasema wanajikakamua kutetea uongozi wao huku wakinuia kurudi katika ligi kuu msimu ujao.

Kadi nyekundu aliyopewa kiungo wa Tottenham Son Heung-min kwa kumgonga Andre Gomes na kumsababishia jeraha baya la mguu, imebatilishwa na F.A.

Awali Son alikua amepewa kadi ya njano kabla ya refa kuibadilisha na kumpa nyekundu. Kiungo huyo wa Korea Kusini aliondolewa uwanjani kwa kucheza vibaya lakini tume huru imetangaza kuwa hakufaa kondolewa. Ligi ya Premier ilieleza kuwa kadi hio nyekundu ilipewa Son kwa kuhatarisha usalama wa mchezaji.

Liverpool itachezesha vikosi viwili tofauti katika mashindano mawili chini ya masaa 24 baada ya EFL kutangaza kuwa tarehe ya mechi yao ya robo fainali ya kombe la Carabao na Aston Villa haitobadilishwa.

The Reds watachuana na Villa tarehe 17 Disemba saa 10:45 usiku na kisha kucheza mechi ya nusu fainali ya kombe la dunia la klabu huko Qatar siku ifuatayo saa 8:30pm.

Meneja Jurgen Klopp alikua amesema hawataweza kucheza mechi hizo. Liverpool sasa watacheza mechi 9 mwezi Disemba.

Chelsea walijikakamua na kutoka nyuma 4-1 na kutoka sare ya 4-4 na kujipatia alama moja muhimu katika ligi ya mabingwa huku Ajax ikimaliza mechi hiyo ugani Stamford Bridge na wachezaji 9.

Ajax walitawala mechi hiyo baada ya  Donny van de Beek kuwafungia mabao matatu dakika 10 baada ya mapumziko lakini Chelsea wakajikakamua na kujiokoa. Cesar Azpilicueta, Jorginho na Reece James walifungia the Blues mabao.

Liverpool walikusanya ushindi mwingine katika kampeni yao kwa kuwanyuka Genk mabao 2-1 ugani Anfield. Vijana wa Jürgen Klopp walipoteza kwa Napoli katika mechi yao ya ufunguzi ya kundi E mechi pekee waliyopoteza msimu huu, lakini wameshinda mechi tatu zilizofuata. Georginio Wijnaldum na Alex Oxlade Chamberlain walifungia Liverpool mabao yao huku mtanzania Mbwana Samatta akiwapa Genk bao moja. Liverpool sasa wapo kileleni mwa kundi lao juu ya Napoli, waliotoka sare ya 1-1 na Salzburg.