Kipchoge, Tiger Woods na Messi kung'ang'ania tuzo la Laureus

eliud.kipchoge
eliud.kipchoge
Bingwa wa dunia katika mbio za marathon kwa wanaume na mtu wa kwanza kukimbia Marathon kwa chini ya masaa mawili Eliud Kipchoge ni miongoni mwa wanamichezo 6 walioteuliwa kwa tuzo la Laureus.

Kipchoge atapambana na Lionel Messi, Rafael Nadal, Lewis Hamilton, Tiger Woods na Marc Marquez kwa tuzo la mwanamichezo bora zaidi duniani. Tuzo hizo zitaandaliwa jijini Berlin, Ujerumani Februari tarehe 17 ambapo Kipchoge alivunja rekodi ya dunia ya Marathon kwa wanaume.

Hayo yakijiri, michuano ya mwaka 2021 ya AFCON itaanza tarehe 9 mwezi Januari baada ya tarehe hio kubadilishwa, waandalizi Cameroon wametangaza.

Kipute hicho kilipangiwa kufanyika mwezi Juni na Julai lakini ikabadilishwa kutokana na hali mbaya ya anga nchini humo wakati huo wa mwaka. Hii ina maana kwamba huenda vilabu vya ligi ya Primia vikakosa wachezaji wa kikosi cha kwanza katika wakati muhimu wa msimu.

Mabadiliko haya yana maana kua kipute hicho hakitakinzana na kombe la dunia la vilabu litakaloandaliwa Uchina mwezi Juni mwaka ujao.

Kwingineko, timu ya Kenya ya mpira wa vikapu ilishinda mechi yao ya pili katika michuano ya Fiba Afro kwa ushindi wa 95 - 59 dhidi ya majirani Tanzania.

Sudan Kusini pia wamesalia kutoshindwa baada ya kuwacharaza Eritrea 111-57. Wakati huo huo Burundi waliwanyuka Somalia 86-106. Kenya sasa watakabana na Somalia saa 6.30 jioni ya leo, huku Eritrea wakichuana na Tanzania, na Burundi wakipambana na Sudan Kusini.