FA CUP: United, Man City na Chelsea wafuzu huku Liverpool wakilemewa

manchester united
manchester united
Jason Cummings alifunga mabao mawili Shrewsbury waliporegea kwa mpigo na kutoka sare ya 2-2 na Liverpool katika raundi ya nne ya michuano ya kombe la FA Cup.

Mabao ya Curtis Jones na la kujifunga la Donald Love yalikua yamemaliza udhia wa viongozi hao wa ligi kabla ya mambo kubadilika. Kwingineko Manchester United walifuzu kwa raundi ya tano kwa ushindi wa 6-0 dhidi ya Tramere huku Manchester City wakiwanyuka Fulham 4-0.

Kiungo wa kati wa Tottenham Christian Eriksen anakaribia kujiunga na Inter Milan, huku akiwa amepangiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu hii leo.

Kiungo huyo wa miaka 27 anatarajiwa kukamilisha uhamisho wa pauni milioni 16.8 kwenda Italia, ambao utampelekea kupata kitita cha hadi pauni elfu 320 kwa wiki. Eriksen amecheza mechi 305 wakati wa tajriba yake ya miaka sita na nusu North London, akifunga mabao 69 na kusaidia 89.

Inter kwa sasa wako katika nafasi ya pili kwenye Serie A, nyuma ya viongozi Juventus. Giovani Lo Celso huenda akachukua nafasi ya Eriksen.

Manchester United wanaweza kumtimua kocha Ole Gunnar Solskjaer iwapo matokeo yao hayataboreka msimu huu, huku kocha timu ya taifa ya Uingereza Gareth Southgate akipigiwa upatu kumrithi Solskjaer.

Kwingineko, Barcelona hawatarajiwi kumsajili mshambuliaji wa Arsenal na Gabon Pierre-Emerick Aubameyang na badala yake wanaelekeza nguvu zao kwa mshambuliaji wa Valencia Rodrigo Moreno.

Bingwa mara sita wa michuano ya Australian Open Roger Federer alitoka nyuma na kufuzu kwa robo fainali jijini Melbourne kwa kumnyuka Marton Fucsovics. Raia huyo wa Swiss alimyuka mwenzake wa Hungary   na atachuana na mwamerika Tennys Sandgren, katika robo fainali hapo kesho, huku bingwa mtetezi Novak Djokovic huenda akasubiri hadi michuano ya wanne bora.