Arsenal, mashetani wekundu wawika ligi ya EPL

Mason Greenwood alifunga mara mbili katika ligi ya premia kwa mara ya kwanza huku Man United ikitoka nyuma na kuilaza Bournemouth 5-2 na kuongeza matatizo ya klabu hiyo inayokaribia kushushwa daraja.

Greenwood mwenye umri wa miaka 18 aliwasawazishia wenyeji baada ya goli lililofungwa na Junior Stanislas kuishangaza Man United kunako dakika ya 15 kabla ya kuifungia United goli lake la nne baada ya kipindi cha kwanza .

Marcus Rashford alikuwa ameiweka United 2-1 juu kutoka mkwaju wa penalti kabla ya Anthony Martial kufunga bao zuri kabla ya kipindi cha kwanza kukamilika.

Katika mechi ilioja mbembwe za kila aina , Joshua King aliifungia timu yake goli la pili kupitia mkwaju wa penalti dakika nne baada ya kipindi cha mapumziko. Kikosi hicho cha Edie Howe , kilifunga goli la kusawazisha ambalo lilikataliwa kwa kuwa la kuotea.

Wakati huohuo Arsenal iliishangaza klabu ya Wolves ugenini na kuimarisha matumaini yake ya kufuzu katika mashindano ya klabu bingwa Ulaya baada ya kuwalaza wenyeji wao 2-0 katika uwanja wa Molineux.

Kinda wa Gunners Bukayo Saka, ambaye alitia saini kandarasi mpya siku ya Jumtano alianza kuifungia klabu yake .

Adama Traore aliharibu nafasi bora zaidi ya kusawazisha , kabla ya Alaxandre Lacazette kuingia kama mchezaji wa ziada na kufunga bao la ushindi.

Arsenal ilipanda hadi katika nafasi ya saba huku ikiwa pointi tatu nyuma ya Wolves.

-BBC