Pigo kwa FKF baada ya akaunti zake kufungwa na mahakama

Shughuli za shirikisho la soka nchini (FKF) huenda zikalemazwa zaidi baada ya mahakama ya kutatua mizozo  ya leba kuzidisha muda wa kufungwa kwa akaunti za shirikisho hilo.

Hatua hiyo ya mahakama inatokana na mzozo wa malipo ya aliyekuwa mkufunzi mkuu wa Harambee Stars Bobby Williamson. Williamson alikwenda mahakamani mwaka 2017  kwa kile alitaja kufutwa kazi kinyume na sheria na rais wa FKF Nick Mwendwa mwaka 2016.

Soma habari zaidi;

Mahakama mwaka jana iliagiza FKF kumlipa fidia na mshahara wake wote.

Agizo la kufungwa kwa akaunti za FKF lilitolewa wiki iliopita na muda huo ukaongezwa tena siku ya Jumatano.

Jaji Byram Ongaya aliagiza ombi hilo kushughulikiwa kama la dharura. Williamson aliwashtaki rais wa FKF Nick Mwendwa na katibu mkuu Robert Muthomi. FKF ilikuwa imeahidi kuwasilisha rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kumtuza Williamson fidia.

Soma habari zaidi;

FKF pia inakabiliwa na vikwazo zaidi kutoka FIFA baada ya kukosa kumlipa fidia aliyekuwa mkufunzi wa Harambee Stars Adel Amrouche shilingi milioni 109 kama ilivyoagizwa na mahakama ya spoti ya FIFA.