Man City yapanda alama 13 kileleni mwa EPL, Gor yalazwa na Nzoia

man city vs west ham , picha kwa hisani ya bbc
man city vs west ham , picha kwa hisani ya bbc

Manchester city ilipanda alama 13 kileleni mwa ligi ya EPL baada ya kuilaza Westham 2-1 jana. Mikhail Antonio alisawazishia the hammers katika kipindi cha pili baada ya Ruben Diaz kuwapa City uongozi, kabla ya mlinzi John Stones kufunga goli la ushindi.

Kwingineko, Leeds ilipoteza 1-0 nyumbani dhidi ya Aston Villa, huku Westbrom wakilaza Brighton  1-0 nao Newcastle walitoka sare ya 1-1 na Wolves. 

Chelsea itaalika mahasidi wao Manchester United  ugani Stamford bridge katika mechi ya kukata na shoka ya EPL, huku pande zote mbili zikiwania ushindi ili kusalia katika kinyanganyiro cha nne bora msimu huu.

Kocha wa the blues Thomas Tuchel atakua anatarajia kuendeleza rekodi yake ya kutoshindwa tangu achukue usukani mwezi uliopita.

Mechi itaanza saa moja unusu. Arsenal nao watapambana na Leicester huku wakiwania kurejea na ushindi ugani King power, baada ya kulazwa na Manchester city wikendi iliyopita. Tottenham nao watacheza dhidi ya Burnley huku Sheffield United wakikaribisha mabingwa watetezi   Liverpool.

Na tukirejea humu nchini Viongozi wa ligi ya FKF Tusker walikosa nafasi ya kupanda alama tisa kileleni mwa ligi baada ya kulazwa 2-1 na wageni Bidco United. Kwingineko, mabingwa Gor Mahia walinyukwa 2-1 na Nzoia Sugar katika uwanja wa Mumias na kuzidi kudidimiza nafasi za kutetea taji lao. Vihiga United nao walitoka sare tasa na Western Stima. 

Aliyekuwa kocha mkuu wa muda katika klabu ya  AFC Leopards Anthony 'Modo' Kimani jana alichukua usukani rasmi kama kocha msaidizi wa timu ya  Bandari. Modo ambaye hapo awali alichezea Ingwe na Mathare United anajiunga na mzaliwa wa Rwanda Cassa Mbungo ambaye alikua mkuu wake wakati mmoja katika klabu ya Ingwe. 

Winga wa Gor Mahia  Nicholas Kipkurui anatarajiwa kujiunga na Ulinzi Stars  baada ya kufuzu katika majaribio ya kuwa mwanajeshi. Kip ambaye alijuinga na KO'gallo mwaka wa 2018 kutoka Zoo Kericho atafanya mafunzo ya kijeshi kwa miezi sita kabla ya kandikisha kandarasi na Ulinzi. Kwa mujibu wa klabu hiyo Kip anatarajiwa kuongeza makali katika safu ya ushambulizi huku wakiwania taji lao la kwanza tangu mwaka wa 2011. 

Huku hayo yakiarifiwa,  Ligi ya FKF itaendelea hii leo huku mechi kadhaa zikipiga katika maeneo mbali mbali nchini.

AFC Leoaprds watakua wanatafuta ushindi wao wa pili mtawalia watakapopiga dhidi ya  Kakamega Homeboyz,huku Ulinzi stars wakinyanyuana na Bandari. KCB  nao wataalika  Kariobangi Sharks huku Posta Rangers wakimaliza udhia dhidi ya Sofapaka.