Jadon Sancho akamilisha uhamisho wa kujiunga na Man United kwa dau la £73m

Muhtasari
  • Jadon Sancho akamilisha uhamisho wa kujiunga na Man United kwa dau la £73m
Image: BBC

Winga wa England Jadon Sancho anasema kwamba kujiunga na Man United ni ndoto iliotimia baada ya kukamilisha uhamisho kutoka klabu ya Borussia Dortmund kwa dau la £73m.

Sancho ndiye mchezaji wa pili wa England mwenye thamani ya juu baada ya mchezaji mwenza wa United Harry Maguire.

Anajiunga na United kwa kandarasi ya miaka mitano.

"Naishukuru Dortmund kwa kunipatia fursa ya kucheza katika kikosi cha kwanza , ijapokuwa , nilijua kwamba nitarudi England'' , alisema Sancho mwenye umri wa miaka 21.

"Fursa ya kujiunga na Manchester United ni ndoto iliotimia na sasa nasubiri kuonesha umahiri wangu katika ligi ya Premia''.

"Hiki ni kikosi kichanga na najua , pamoja tunaweza kujenga kitu maalum ili kuleta ufanisi ambao mashabiki wanahitaji.."

United waliafikia makubaliano ya kumsajili Sancho tarehe mosi mwezi Julai na kandarasi yake ya miaka mitano na klabu hiyo ina kifungu cha miezi mingine 12.

Ukamilishaji wa makubaliano hayo unasitisha uwindaji wa kumsajili mchezaji huyo. Walitarajiwa kumsajili msimu uliokwisha lakini wakatofautiana kuhusu dau la uhamisho wake.

Sancho alifunga magoli 50 na kutoa usaidizi wa magoli 57 katika mechi 137 alizochezea Dortmund.

Mkufunzi wa United Ole Gunnar Solskjaer anasema kwamba Old Trafford itampatia Sancho , fursa anayohitaji kuonesha talanta yake.

"Jadon ni aina ya mchezaji ambaye nilipenda kumleta katika klabu hii - ni mshambuliaji anayeingiliana na utamaduni wa Man United'' , Solskjaer aliambia tovuti ya klabu hiyo.

"Atakuwa kiungo muhimu wa kikosi changu kwa miaka kadhaa ijayo na tunataraji kwamba atang'ara. Magoli yake na rekodi yake ya usaidizi wa magoli ni ya kipekee na pia atatuongezea kasi katika mchezo wetu , umahiri na ubunifu katika timu."

Kurudi kwa Sancho katika ligi ya Uingereza kunajiri baada ya kuisadia timu ya taifa kufuzu katika fainali ya kombe la Yuro 2020 , ambapo walishindwa na Itali kwa penalti.

Mchezaji huyo wa zamani wa Kikosi cha vijana cha timu ya Man City pamoja na Bukayo Saka na Marcus Rashford walikabiliwa na ubaguzi wa rangi katika mitandao ya kijamii baada ya kushindwa kufunga penalti muhimu walizopewa.