Mshambulizi matata Romelu Lukaku amerejea ligi kuu ya Uingereza miaka miwili tu baada ya kuhamia ligi ya Serie A nchini Italia.
Lukaku, 28, hajarejea Uingereza tu mbali amejiunga na klabu ya Chelsea ambayo aliwahi kuichezea kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mshambulizi huyo ambaye aliondoka Chelsea mwaka wa 2014 ametia saini mkataba wa miaka mitano na washindi hao wa ligi ya mabingwa msimu uliopita.
Chelsea ilitoa tangazo hilo kupitia tovuti rasmi ya klabu jioni ya Alhamisi.
Alipokuwa anathibitisha kusajiliwa kwake, Lukaku alisema kuwa ni furaha yake kurejea kwa klabu aliyoiunga mkono tangu utotoni.
"Nina raha sana. Imekuwa safari kubwa kwangu. Nilikuja hapa kama mtoto ambaye alikuwa na mengi ya kusoma na sasa nimerudi nikiwa na uzoefu mkubwa" Lukaku alisema.
Welcome home, @RomeluLukaku9. 💙#LukWhosBack pic.twitter.com/P43CAIVqfU
— Chelsea FC (@ChelseaFC) August 12, 2021
Mkurugenzi wa Chelsea Marina Granovskaia alisema kuwa ni furaha ya klabu kumsajili Lukaku kwani ataongeza talanta kubwa kwenye kikosi chao.
"Lukaku ni miongoni mwa washambulizi na wafungaji bao bora duniani. Tumefurahia sana kumrejesha kwa klabu anayoipenda and tuna raha kuongeza talana kwa kikosi chetu" Marina alisema.
Inaripotiwa kuwa Lukaku ambaye amekuwa katika klabu ya Inter kwa kipindi cha misimu miwili amesajili kwa takriban pauni milioni 97.5
Mbali na Chelsea na Inter, Lukaku aliwahi kuchezea Anderlecht ya Ubelgiji, West Brom, Everton na Manchester United.
Kwa sasa mchezaji huyo ameandikisha mabao 113 katika ligi kuu ya Uingereza na ameorodheshwa kama nambari 20 kwenye orodha ya wafungaji bora wa wakati wote.
Ameifungia timu ya Ubelgiji mabao 64 katika mechi 98 ambazo amechezea timu ya taifa lake.