Shughuli zote za ligi za FKF nchini zimesimamishwa

Muhtasari
  • Kamati mpya ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) imesimamisha shughuli zote za kandanda kote nchini mara moja
Aaaron Ringera
Image: Hisani

Kamati mpya ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) imesimamisha shughuli zote za kandanda kote nchini mara moja.

 Aaron Ringera aliyeongoza kamati ya muda, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa Ijumaa, Novemba 12, ilisema kwamba shughuli zote za soka za ngazi ya juu zitasitishwa mara moja.

Haya yanajiri kufuatia mjadala uliotolewa na kamati hiyo baada ya kuteuliwa ofisini na Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Michezo, Amina Mohamed.

Shughuli zilizosimamishwa ni pamoja na Ligi Kuu ya FKF, Ligi Kuu ya Kitaifa ya FKF, FKF Daraja la Kwanza, Ligi Kuu ya Wanawake ya FKF, na Ligi ya Divisheni ya 1 ya FKF ya Wanawake.

Kamati hiyo inatarajiwa kuwasiliana na vilabu na wadau wengine wa soka kabla ya kutoa mapendekezo zaidi.

Hata hivyo, ligi zinazoendeshwa chini ya matawi zitaendelea kama kawaida.

"Tunataka kuwahakikishia wapenzi wote wa soka ya Kenya kwamba kamati itahakikisha utendakazi mzuri wa shughuli zote za kandanda kote nchini na kwingineko," kamati hiyo ilisema.

Uahirisho ambao utaanza kutumika mara moja utaendelea kwa muda wa wiki mbili, kuanzia leo.

"Uamuzi umefikiwa ili kuhakikisha uratibu wa shughuli za ligi nchini kote,Kamati itakuwa ikishirikiana na vilabu na wadau wengine wa soka kwa wakati muafaka,"Ringera alisema katika taarifa.