Mji wa Iten nchini Kenya umekumbwa na mauaji kwa mara ya pili ya mwanariadha wa kike katika muda wa miezi sita.
Mauaji ya Damaris Muthee Mutua, 28, ambayo yaliripotiwa wiki jana yalijiri baada ya mshindi wa medali ya shaba mara mbili wa Riadha za Dunia Agnes Tirop kupatikana akiwa amedungwa kisu hadi kufa Oktoba mwaka jana.
Mutua, mama wa mtoto mmoja, hakuwa na wasifu wa Tirop lakini kifo chake kimezidisha wasiwasi kuhusu mauaji ya wanawake na usalama wa wanariadha wa kike katika nchi hiyo ya Afrika mashariki.
Mutua alizaliwa nchini Kenya na akabadili kuwania ushindi kupitia nchini ya Bahrain, lakini alipata mafunzo huko Kapsabet, mji ulio kati ya Iten na Eldoret, na ulioko katika eneo la Kenya maarufu kwa kuzalisha na kulea wakimbiaji wa mbio ndefu.
Siku ya Alhamisi, polisi wa Kenya walisema kuwa uchunguzi wa maiti yake ulibaini kuwa kifo chake kilitokana na kunyongwa koo, huku uchunguzi wa sampuli za tumbo pia ukichukuliwa ili kubaini kama kulikuwa na mchezo mchafu zaidi.
Mnamo mwaka 2010, Mutua alishinda shaba kwa nchi yake ya Kenya katika mbio za mita 1,000 katika Michezo ya Olimpiki ya Vijana nchini Singapore.
Msimu wake bora zaidi ulikuja mnamo 2018 alipokimbia mbio-bora kwa kilomita 20 (saa moja, dakika nane na sekunde 28 - wakati bora zaidi wa mwaka) aliposhinda mbio huko Marrakesh, na vile vile nusu-marathon (1: 11:51), akimaliza wa pili katika hafla moja huko Msumbiji.
Alikuwa amefurahia mwanzo mzuri wa mwaka 2022, akichukua nafasi ya pili katika Mashindano ya Nchi za Kiarabu ya mbio za cross country nchini Bahrain mwezi Februari kabla ya kushika nafasi ya tatu kwenye nusu-marathon ya Luanda nchini Angola mapema Aprili.
''Alikuwa mkimbiaji mzuri anayecipuza. Watu wangemtaja kama mtu mwenye nidhamu nzuri,'' Elias Makori, mhariri mkuu wa michezo katika televisheni ya Nation Media Group, aliiambia BBC Sport.
''Mapema mwezi huu, alikuwa wa tatu katika mbio ngumu sana za nusu marathon nchini Angola. Alipatikana akiwa amefariki dunia wakati taaluma yake ndio imeshika kasi."
'Maisha yake yamekatizwa'
Msako unaendelea wa kumtafuta mwanamume aliyekuwa mpenzi wa Mutua kutoka Ethiopia, ambaye alifanya mazoezi katika kituo kimoja cha mwinuko, huku mwanariadha huyo ambaye pia ni marehemu akiwa na mtoto wa kiume kutoka kwa ndoa yake na Mkenya Felix Ngila.
''Tumehuzunika - ameacha mtoto wa miaka sita,'' baba mkwe wa Mutua Josephat Ngila Ndeti alisema Alhamisi.
''Naiomba Serikali ifanye kazi yake vizuri na kujua mhusika yuko wapi. Hatuwezi kupata kitambulisho chake wala hati zake za benki, zote zilikuwa ndani ya nyumba. Nani amezichukua?''
Aliuliza.
Riadha Kenya ilisema ''imehuzunishwa sana'' na kifo chake.
''Ni kisa kingine cha kukatizwa kwa maisha na talanta ikaharibiwa kwa kuzingatia mafanikio ambayo Damaris alikuwa amepata katika taaluma yake,'' taarifa kutoka kwa bodi iliongeza.
''Ingawa alikuwa amebadili utiifu, Damaris alikuwa Mkenya kwa damu. Kufariki kwake ni uchungu zaidi ikizingatiwa hii si mara ya kwanza kwa mustakabali mzuri kukatizwa na unyanyasaji wa nyumbani.''
Riadha Kenya imekumbwa tena na masuala yanayokumba baadhi ya wanariadha wa kike, ambao wana wasiwasi kuhusu unyanyasaji wa nyumbani, masuala mengine ya ndoa, na jukumu la makocha wa kiume kuwanyanyasa wanariadha.
''Ni [kifo cha Mutua] kinakuja baada ya mfululizo wa kliniki za uhamasishaji kufanywa kote nchini ili kuwapa wanariadha usaidizi wa kimaadili na kuangalia afya yao ya akili, ambalo ni suala linalotia wasiwasi mkubwa,'' Makori alisema.
''Tulipofikiria kuwa mambo yangebadilika kuwa bora, hili likafanyika.''