ATAKA KUWA MKUFUNZI

Mwanabondia Nick Okoth astaafu

BFK ilisema mwanabondia huyo atakoswa pa kubwa na wapenda ndondi nchini.

Muhtasari

•BFK ilisema Okoth ameacha pengo kubwa ambalo litachukua muda kuziba.

•Uongozi huo wa masumbwi nchini ulimtakia mafanikio bondia huyo anapoingia kwenye changamoto mpya ya kukuza vipaji.

Bondia Nick Okoth
Bondia Nick Okoth
Image: BFK

Shirikisho la ndondi nchini Kenya limempongeza nahodha mkongwe wa Hit Squad Nick Okoth kwa kupigania taifa kwa ushujaa kwa takriban miongo miwili.

BFK ilisema mwanabondia huyo atakoswa pa kubwa na wapenda ndondi nchini na ugaibuni waliofurahia ujasiri wake ulingoni.

"Vema na asante nahodha Nicholas Okoth kwa nyakati nzuri za michezo na burudani isiyo na kikomo ambayo umetupa kutazama ukiwakilisha klabu na nchi kwa miaka mingi," BFK ilisema.

 

BFK ilisema Okoth ameacha pengo kubwa ambalo litachukua muda kuziba. "Umekuwa mwanaspoti mzuri! washindani wako, mashabiki, BFK na mchezo wa ndondi, kwa ujumla, hakika watakukosa.”

Uongozi huo wa masumbwi nchini ulimtakia mafanikio bondia huyo anapoingia kwenye changamoto mpya ya kukuza vipaji.

"Unapostaafu na kuchukua jukumu lako mpya kama mkufunzi, hatukutakii chochote ila bora."

Katika mahojiano ya kipekee mwezi uliopita, Okoth alikiri kwamba umri ulimnyima hamu ya kuendelea zaidi. Alisema atatumia miaka yake iliyosalia kukuza vipaji vya kizazi kipya cha mabondia wa Kenya.

Okoth, 39, aliyepeperusha bendera ya nchi kwenye Mashindano ya Ndondi ya Afrika mjini Maputo, Msumbiji mwezi uliopita, alisema mchuano huo uliadhimisha safari yake ya mwisho ulingoni.

"Imetosha. Sina tena nguvu ya kupambana na damu changa na changamfu,” Okoth alisema.

“Sasa ni wakati wa kuandaa njia kwa mabondia chipukizi. Tunachohitaji sasa ni kuingia kwenye dimbwi la vipaji na kukuza kizazi kipya. Nimeona idadi kubwa ya mabondia wajao wenye uwezo wa kuiletea nchi yetu ushindi,” aliongeza.

 

Mnamo Mei 26, Okoth alidokeza kustaafu baada ya Michezo ya Jumuiya ya Madola ya Birmingham 2022 nchini Uingereza lakini akabadili uamuzi wake.

Okoth alieleza ni kwa nini alibadili nia. "Nilipohudhuria majaribio ya kitaifa baada ya michezo ya Birmingham, nilitarajia kupata kijana ambaye angenitoa nje ya uzani wa flyweight lakini hakuna aliyekuwepo," Okoth alisema.

"Mtu asitarajie kupata nafasi katika timu ya kitaifa kwa njia rahisi. Ni sharti kila moja apiganie nafasi yake katika kikosi cha Hit Squad,” aliongeza.

Okoth aliwataka mabondia hao chipukizi kuepuka kutumia vitu vinavyoweza kudhoofisha mfumo wa miili yao na kuharibu kazi yao.

“Nimegundua kuwa mabondia wengi wanaokuja wanajiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya. Mielekeo kama hii itatumika tu kuharibu juhudi zozote wanazoweza kuweka," Okoth alisema.

Okoth alielezea furaha yake baada ya kujinyakulia medali ya fedha katika onyesho la bara la Maputo ambapo pia alijipatia Sh600,000 kutokana na ushujaa wake ulingoni.

"Maputo ilikuwa ubingwa wangu wa tatu wa Afrika na ninashukuru sana kuwa na nafasi kama hiyo. Nilishinda medali mbili za dhahabu katika matembezi yangu ya awali na nilikuwa na matumaini ya dhahabu nyingine. Hata hivyo, bado nashukuru kwa fedha hizo," Okoth alisema.

Okoth alikosa taji la uzani wa lightweight baada ya kushindwa na Chilata Andrew wa Zambia.

Alitinga fainali baada ya kumuangamiza Walid Tarzout wa Algeria katika mchezo wa pili. Alikuwa ametinga nusu fainali kufuatia ushindi mnono wa 5-0 dhidi ya Jean Jerry Agathe wa Mauritius katika robo fainali.