Mchezo wa NFL wasimamishwa baada ya mchezaji kuanguka uwanjani

Hamlin alipelekwa katika hospitali na yuko katika hali mbaya.

Muhtasari

•Hamlin alianguka chini katika robo ya kwanza ya mchezo baada ya kugongana na Tee Higgins wa Bengal.

Image: BBC

Mchezo wa Ligi ya Taifa ya Soka ya Marekani umesimamishwa baada ya mchezaji wa Buffalo Bills Damar Hamlin kuzimia wakati wa mchezo dhidi ya Cincinnati Bengals.

Hamlin, 24, ambaye anacheza nafasi ya usalama, alianguka chini katika robo ya kwanza ya mchezo baada ya kugongana na Tee Higgins wa Bengal.

Amepelekwa katika hospitali ya eneo hilo na yuko katika hali mbaya, NFL ilisema.

Wachezaji walionekana wakitokwa na machozi na kukumbatiana katika maombi ya pamoja kwa ajili ya Hamlin.

Ripota wa michezo nchini Joe Danneman aliandika kwenye Twitter kwamba aliambiwa Hamlin "ana mapigo ya moyo, lakini hapumui peke yake".

Maafisa wa matibabu walikuwa wamempa CPR mchezaji huyo uwanjani mara moja kabla ya kumpeleka kwenye gari la wagonjwa, ESPN iliripoti.

Waandaaji waliafikia uamuzi wa kusimamisha rasmi mchezo huo kwa usiku huo takriban saa moja baada ya tukio hilo. Michezo ya NFL mara chache husimamishwa kwa sababu ya jeraha.

Chama cha wachezaji wa ligi hiyo kiliandika katika taarifa: "Tumekuwa tukiwasiliana na wachezaji wa Bills na Bengals, na NFL. Kitu pekee ambacho ni muhimu kwa wakati huu ni afya na ustawi wa Damar."