Julian Nagelsmann anaelekea kutimuliwa kama kocha mkuu wa klabu ya Bayern Munich, huku meneja wa zamani wa PSG na Chelsea, Thomas Tuchel akitarajiwa kuchukua nafasi yake.
Ripoti kutoka Ujerumani zinasema kuwa Mabingwa hao mara 31 wa Bundesliga tayari wamefikia makubaliano na kocha huyo Mjerumani mwenye umri wa miaka 49 na anatarajiwa kutangazwa kama meneja mpya mnamo Ijumaa, Machi 24.
Klabu hiyo pia inatarajiwa kuthibitisha kutimuliwa kwa Nagelsmann ambaye amehudumu kama kocha wake kwa karibu miaka miwili. Mkufunzi huyo ambaye hakuwepo uwanjani wa mazoezi wiki hii, anatarajiwa kukutana na wakurugenzi wa Bayern siku ya Ijumaa wakati ambapo atafahamishwa rasmi kuhusu uamuzi huo.
Mabingwa hao wa Bundesliga wanatatizika katika ligi ya nyumbani msimu huu na wako nafasi ya pili nyuma ya Borussia Dortmund.
Tuchel amekuwa nje ya kazi tangu alipotimuliwa na klabu ya Chelsea mwezi Septemba baada ya Mmarekani Todd Boehly kuchukua umiliki wa klabu. Amekuwa akiishi jijini Munich, Ujerumani kwa muda tangu kutimuliwa kwake.
Hapo awali, aliwahi kuwa meneja wa PSG, Borrusia Dortmund, FSV Mainz na FC Ausburg II. Akiwa Chelsea, Mjerumani huyo alisaidia klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza kutwaa taji la kifahari la Kombe la Mabingwa.
Wachezaji wa Bayern Munich wanaonekana tayari kuwa na ufahamu kuhusu mabadiliko ambayo yanaendelea katika klabu hiyo.
Beki wa Manchester City, Joao Cancelo, ambaye kwa sasa yuko Bayern kwa mkopo tayari amemkaribisha Tuchel kwenye klabu hiyo.
"Nimegundua sasa hivi, najua sitampata Nagelsmann nitakaporudi Munich - alitaka niende Bayern, ningependa kumshukuru," Beki huyo wa timu ya taifa ya Ureno alisema kwenye mahojiano siku ya Alhamisi.
Aliongeza, "Kuhusu Tuchel, alinifanya nipoteze fainali ya Ligi ya Mabingwa, kwa hivyo natumai atanishindia mwaka huu!".
Bayern, ambao wametajwa kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mwaka huu wanatarajiwa kumenyana na Mabingwa wa EPL, Manchester City Aprili 11 na Aprili 17. Akiwa ameshinda kombe hilo na Chelsea miaka michache tu iliyopita, itakuwa ya kuvutia kuona iwapo kocha huyo mwenye umri wa miaka 49 atainyanyua akiwa na klabu hiyo ya Ujerumani.